MAGONJWA
YA VIAZI MVIRINGO
UTANGULIZI:
Maana:
Ugonjwa ni hali ambayo hutokea baada ya
sehemu mojawapo ya mmea kushambuliwa na vijidudu au vimelea visababishavyo
ugonjwa, hali ambyo husababisha kudhoofika kwa mmea na kushindwa kufanya au
kuota vizuri. Kwa kawaida magojwa hayo husababishwa na vijidudu au vimelea
kutoka kwa Fangasi, bakteria na virusi,au minyoo fundo ambayo ni viumbe ndogo
zaidi visivyoweza kuonekana hata kwa jicho.
AINA
ZA VIMELEA/VIJIDUDU
Fangasi
– Hawa ni vimelea kwa sura vinaonekana kana nyuzu nyuzi ambazo huzaliana kwa
kutoa unga unga (spores). Vijidudu hivi vinaweza
kuingia kwenye mimea
kikamilifu kupitia vidonda, mashimo ya asili katika mimea, kubebwa na wadudu,
au kuingia moja kwa moja wakati wa kupanda. Magonjwa yasababishwayo na vimelea
hivi yanaweza kuenea kwa njia ya maji, udongo, upepo na mbegu na juu ya zana za
kilimo. Mfano wa ugonjwa unaosababishwa na fangasi kwenye viazi ni ugonjwa wa
ukungu au baka jani chelewa.
Bakteria
– Hivi ni vimelea vidogo vidogo kuliko fangasi, vina uwezo wa kuzaliana kwa
spores na kugawanyika vyenyewe. Huzaliana sana hasi vinapokuwa kwenye hali
nzuri na mazingira mazuri ya kuzaliana. Bakteria huingia ndani ya mimea kupitia
vidonda na mashimo ya asili au kusafirishwa na wadudu. Magonjwa
yanayosababishwa na bacteria hasa kwa viazi ni mnyauko bakteria na kuoza kwa
viazi vyenyewe.
Virusi
- Virusi ni vijidudu/vimelea vidogo sana kuliko hata fangasi na bakteria. Hivi
vimelea Haviwezi kuishi kwa kujitegemea lazima pawepo na kiumbe hai hasa mmea
unaoruhusu kirusi kuishi na kuweza kuzaliana kwa wingi.
Virusi huenea kutoka mmea mmoja na
mwingine kwa njia ya kupanda mbegu zilizokwisha ambukizwa, au na wadudu kama
vile wadudu mafuta na nzi weupe.
Viwavi
(Nematodes) - Viwavi ni vijidudu umbo kama minyoo
midogo midogo. Minyoo hii huathiri mimea na kusababisha mmea kufa. Viwavi
vinaweza kuenea kikamilifu na kwa haraka kwa njia ya udongo, maji na upepo, au
zana za kilimo pembejeo na mbegu.
Magonjwa yote ni vigumu zaidi kuweza
kuyatambua au kuyachunguza kuliko wadudu ndani ya mimea, hii ni kutokana mara
nyingi magonjwa mengi hayaonekani kwa macho ya kawaida. Kwa mkulima kuweza
kutambua kwamba kuna ugonjwa ndani ya shamba, ni mpaka aone dalili Fulani
tofauti kwenye mmea ambazo si za kawaida.
Jinsi
ya kupambana na magonjwa ya mimea
Kanuni
za kujikinga na magonjwa
Kwa kawaida ili ugonjwa uweze kutokea na
kushambulia mimea shambani, ni lazima pawepo na vitu vitatu. Vitu hivyo ni
Vijidudu/vimelea vya kusababisha ugonjwa, hali au mazingira yanayoruhusu
kustawi kwa vimelea hao, pamoja na mmea wenyewe. Mambo haya matatu yanahusiana
na kutegemeana kila mmoja na mwenzake.
Yakufanya ili ugonjwa usizuke na
kushambulia mimea ni kama yafuatayo:-
1.
Kuzuia chanzo cha vimelea.
• Kufanya usafi wa mazingira
·
Kuharibu mabaki ya mimea inayowezi
kuambukiza ugonjwa
·
Kuchagua mashamba yasiyo na historia ya
magonjwa
·
Kama ni kilimo cha umwagiliaji, tumia
maji safi kwa ajili ya umwagiliaji na
·
Kutumia mbegu za viazi zisizokuwa na
magonjwa
·
Kutumia kilimo mzunguko wa mazao.
2.
Kutumia mmea husika:
·
Kwa kutumia mbegu za viazi zilizo safi
na bora zenye ukinzani wa magonjwa mbalimbali.
·
Matumizi ya viwango sahihi vya mbolea.
·
Kupanda kwa majira sahihi ili kuepukana
na milipuko ya magonjwa
3.
Sambamba na mabadiliko ya hali ya
mazingira:
·
Kupanda viazi mwishoni mwa msimu wa mvua
au mwishoni mwa msimu wa ukame.
Kudhibiti
kwa kutumia viumbe hai
Kama ilivyo kwa wadudu, magonjwa pia
yana maadui wanaozuia magojwa au vimelea vya magonjwa visiweze kustawi. Vimelea
au bacteria wanaopatikana kwenye udongo wanaweza pia kutumika kwa ajili ya
kuzuia magonjwa mbalimbali ya mimea. Mkulima anashauriwa kutumia mbolea asili
ili kuweza kuongeza wingi wa viumbe hai kwenye udongo. Baadhi ya vimelea
hutengenezwa na kuuzwa kwa ajili ya kutokomeza vimelea wengine ndani ya udong.
Kwa mfano adui Kuvu Trichoderma ambaye ni Kuvu husaidia hupunguza fangasi
nyingine wanaotokana na udongo.
Kudhibiti
kwa kutumia kemikali za viwandani
Katika kilimo cha viazi mviringo, bado
ni vigumu kuondoa matumizi ya madawa ya kuulia wadudu na kuzuia magonjwa. Hii
inatokana na kuongezeka kwa vimelea vya magonjwa na wadudu shambani kwa sababu
ya mabadiliko ya tabia nchi. Wakulima wengi wa viazi mviringo hutumia sana dawa
za kuzuia ugonjwa wa ukungu, lakini jinsi ya kutumia na wakati gani pamoja na
aina gani ya kiua kuvu kitumike, bado ni tatizo
kwa baadhi ya wakulima kama siyo wote. Tabia hiyo husababisha upinzani
kwa vimelea wa ugonjwa husika, pia na mabaki ya madawa kusababisha sumu ndani
ya viazi na kwa mazingira kuharibika. Kwa sababu hiyo, mbinu bora ya udhibiti
wa magonjwa ni muhimu.
MAGONJWA
MUHIMU YANAYOSUMBUA KWENYE VIAZI MVIRINGO
Magonjwa
yanayosababishwa na vimelea bacteria
1. Mnyauko bakteria (Bacterial wilt)
Ni ugonjwa unaosababishwa na kimelea
kiitwacho kwa lugha ya kitaalam Ralstonia
solanacearum. Kimelea hiki hushambulia si tu viazi mviringo bali hata na
mimea yote jamii ya viazi kama vile pilipili, nyanya, tumbaku na bilinganya,
Ugonjwa huu ni hatari sana, hasa katika maeneo ambako viazi mviringo vinalimwa.
Ugonjwa huu hupunguza kiasi cha mavuno ya viazi mviringo hata kufikia asilimia
90, Wakulima wengi hutumia madawa ya kuzuia ukungu ili kudhibiti ugonjwa huu
bila mafanikio kwani ugonjwa huu hautibiwi kwa dawa yoyote.
DALILI
ZA UGONJWA WA MNYAUKO BACTERIA
Dalili za maambukizi ya ugonjwa wa
mnyauko bakteria zinaweza kuonekana sehemu ya juu ya mimea ulioambukizwa.
Dalili huanza kuonekana kwenye incha za majani kisha mmea huanza kunyauka wote
au baadhi ya mashina. Dalili nyingine hujitokeza kwenye mizizi na mashina,
ambapo mkulima anaweza kuzitambua kwa kukata shina na kuangalia ndani ataona michiriizi
ya rangi ya kahawia. Kama ikitokea mmea ukawa na viazi tayari, basi mkulima
anaweza kuona majimaji yanatoka kwenye macho ya kiazi, hali hii husababisha
udongo kugandamana kwenye macho ya kiazi, hata hivyo mkulima anaweza
kudhibitisha kwa kukikata kiazi na kukiangalia kwa ndani ataona michirizi ya
rangi ya kawia. Hii inatosha kumwonesha mkulima kuwa viazi vyake au shamba lake
lina ugonjwa wa mnyauko bakteria. Kiazi kilichaambukizwa na ugonjwa pia
huonesha dalili za kuoza.
Njia nyingina ambayo anaweza kuitumia
mkulima, ni kuchukua glasi iliyojaa maji masafi, kisha kukata kipande cha shina
la mmea ulioambukizwa na kukining’iniza ndani ya maji, ataona ute mweupe
unashuka ndani ya maji kutoka kwenye lile shina.
Nini
chanzo cha kuenea kwa ugonjwa huu?
Mimea ya viazi mviringo huweza kupata
maambukizi ya ugonjwa wa myauko bacteria kutoka kwenye;-
1.
Udongo – Vimelea vya ugonjwa huweza
kuishi ardhini kwa muda mrefu.
2.
Maji ya mvua au kumwagilia
3.
Mbegu zilizo athrika tayari
4.
Magugu yatunzayo vimelea vya ugonjwa
5.
Mabaki ya viazi au mimea ya viazi
mviringo
6.
Zana za kilimo zitumikazo shambani na
mifugo
JINSI
YA KUDHIBITI UGONJWA WA MNYAUKO BAKTERIA
Ugonjwa wa mnyauko bacteria hauwezi
kudhibitiwa na madawa ya kuzuia ukungu kama wakulima wengi wanadhani. Dawa
halisi ya kudhibiti ugonjwa huu haipo sana madukani, n ahata hivyo dawa
ikipatikana huuzwa ghali, kiasi cha kumfanya mkulima kushindwa kumudu. Kimsingi
ugonjwa wa mnyauko bacteria unaweza kudhibitiwa kwa kufanya haya yafuatayo:-
1.
Kupanda viazi mviringo kwenye shamba lisilokuwa
na vimelea vya ugonjwa.
2.
Kutumia mbegu safi zisizokuwa na ugonjwa
hasa mkulima anashauriwa kununua mbegu kutoka kwa wazalishaji wataalam wa mbegu
za viazi mviringo.
3.
Kutumia kilimo cha mazao mzunguko na
mazao mengine yasiyo ya jamii ya viazi. Kwa mfano;- Mazoezi mazuri ni mzunguko
wa viazi na mahindi au ngano au carrot.
4.
Kuondoa mabaki ya viazi na mimea ya
viazi mara tu baada ya kuvuna.
5.
Kusafisha zana za kilimo baada ya
kutumia.
2. Upele upele mweusi (Common scab)
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na fangasi
aitwaye kwa jina la kitaalam kama Streptomyces scabies, ni maarufu
kwenye udongo wenye tindikali ndogo (low pH). Ugonjwa huu hauna madhala makubwa
kwa upande wa mavuno ya viazi, hata hivyo, unaathiri muonekano wa viazi
vyenyewe, na hivyo kupunguza ubora. Kwa wazalishaji wa mbegu ni vema wakajua
namna ya kukabiliana na ugonjwa huu, kwani unasababisha kupungua kwa ubora wa
mbegu, kisha kupunguza hata bei ya kuuzia.Pia
huathiri hata kwa wauzaji wa viazi vya kusindika viwandani na wale wanao
safirisha nje ya nchi.
DALILI
ZA UGONJWA WA MAPELE MEUSI
Dalili zake huonekana kwenye kiazi
chenyewe, viazi hupasuka ngozi, na mwishowe kuwa na madoa meusi kwenye ngozi ya
kiazi.
Chanzo
cha maambukizi
Ugonjwa huu unaweza kuambukizwa kutoka
kwenye udongo, mbolea aina ya mboji au mbegu za viazi zilizoathrika tayari au
maji yanayotumika kwa kumwagilia.
Jinsi
ya kudhibiti Ugonjwa
Unaweza kudhibiti ugonjwa wa mapele kwa
kufanya yafuatayo:
1.
Kuepuka kupanda katika mashamba yenye
tindikali kidogo, au kwa udongo wenye tindikali kidogo, mkulima anashauliwa
kuongeza madini ya chokaa.
2.
Kwa kutumia mbegu iliyo safi na bora.
3.
Kutumia mazao mzunguko
4.
Kutokomeza kabisa mabaki ya mimie ndani
ya shamba lililoathirika.
3. Ugonjwa wa ukungu au Kuvu (Late
blight)
Huu ni ugonjwa muhimu Zaidi kwa wakulima
wa viazi mviringo. Ugonjwa huu husababishwa na fangasi aina ya Phytophthora
infestans, na kuathiri mazao ya viazi mviringo katika Nyanda za
kitropiki. Mara kwa mara husababisha kudhoofika kwa mazao shambani, mimea
hupata ugonjwa huu mara tu baada ya kuota mpaka wakati wa mavuno. Maambukizi
mengi hutokea katika nyakati za mvua kubwa, unyevunyevu mwingi na na kipindi
cha baridi kali. Wakulima wengi hutumia viua kuvu kwa ajili ya kudhibiti
ugonjwa huo.
Dalili
za ugonjwa wa Ukungu
Dalili za ugonjwa huu hutokea hasa
kwenye majani, shina na kwenye viazi vyenyewe. Majani yaliyoathirika huonekana
kama yaliyochubuka au kama yaliyowekwa kwenye maji ya moto. Hali hii hupelekea
majani hayo kuoza na kukauka. Wakati maambukizi bado ni hai, unga mweupe
huonekana chini ya majani, na mashina yaliyoambukizwa huanza kuoza kuanzia juu
kwenye teke teke, na hatimaye kukauka. Viazi vilivyathrika na ugonjwa wa ukungu
huonesha rangi ya kawia kwenye ngozi. Maambukizi yakiwa makubwa sana, na dawa
ya kudhibiti ikicheleweshwa, mazao yaweza kuharibika ndani ya siku mbili au
tatu.
Chanzo
cha maambukizi
Ugonjwa wa ukungu unaweza kuambukizwa
kwa njia ya hewa, udongo, maji, mbegu na mabaki ya mimea iliyoambukizwa. Huenea
kwa haraka sana kupitia njia ya hewa, udongo, maji na mbegu zilizoathrika. Poda
nyeupe juu ya uso wa majani yalioathirika inaweza kubebwa na upepo na kueneza
ugonjwa kwa mimea mingine.
Jinsi
ya kudhibiti ugonjwa wa Ukungu
Mambo muhimu ya kuzingatia ili kuweza
kudhibiti ugonjwa huu ni kufanya haya yafuatayo;-
(1) Matumizi ya mbegu za viazi zenye
ukinzani
(2) Kufanya uchunguzi wa shamba mara kwa
mara ili kugundua ugonjwa kama upo
(3) Kutumia Mbegu safi isiyo na ugonjwa
(4) Kutumia kilimo mzunguko wa mazao.
(5) Kupanda mbegu za muda mfupi
(6) Kukata majani ya viazi siku 90 baada
ya kupanda
(7) Matumizi ya madawa ya kuzuia na
kutibu ukungu. Mkulima anashauriwa kutumia madawa ya kuzuia ukungu kama vile
farmerzeb au sunstar au ridomil. Iwapo ugonjwa utaonekana tayari shambani, basi
anaweza kutumia dawa kama Linkomil au Ridomil yenye kiambatanisho cha
metalaxiyl. Dozi iliyopendekeza kwa dawa za ukungu ni 2.5 g ya dawa kwenye lita
moja ya maji.
VIRUSI
VYA VIAZI MVIRINGO
Kama ilivyo kwisha elezewa hapo mwanzo,
Virusi ni vijidudu/vimelea vidogo sana kuliko hata fangasi na bakteria. Hivi
vimelea Haviwezi kuishi kwa kujitegemea lazima pawepo na kiumbe hai hasa mmea
unaoruhusu kirusi kuishi na kuweza kuzaliana kwa wingi. Wao wanahitaji kuishi
ndani ya mimea ili kukamilisha maambukizi mzunguko wao. Kwa wakulima wa viazi,
ugonjwa wa virusi ni hatari sana kwani mara unapokuwa ndani ya mbegu za viazi,
magonjwa yasababishayo na virusi hupunguza mavuno kutoka kizazi kimoja hadi
kingine. Virusi hivi huishi ndani ya mbegu za viazi mviringo na hali hiyo
hupelekea mbegu kuota kwa shinda hata kupunguza mavuno. Virusi vinapokuwa ndani
ya mbegu dalili zake huwa ni vigumu kwa mkulima kuzitambua
Ni vigumu kwa wakulima kupata uelewa wa
magonjwa ya virusi kwa sababu:
• vimelea hivyo ni vidogo sana na siyo
rahisi kuviona kwa macho.
• Maambukizi ya virusi ni nadra
kusababisha mimea kufa. Dalili za wazi, kama mimea imeambukizwa na virusi, ni
mabadiliko katika mwonekano wa mimea shambani. Hali hii hupelekea mavuno ya
viazi kuwa na viazi vyembamba. Wakulima wengi wakati wa kuandaa mbegu za msimu
unaofuata, huchagua mbegu ndogo ndogo, hivyo hata huzaaji wake huwa dhaifu
kwani tayari zinakuwa zimebeba virusi.
Kuna aina kama sita za virusi wa viazi
waliokwisha tambuliwa kwa hapa Tanzania. Aina hizo hutoa dalili zinazofanana,
hata kupelekea ugumu wa utambuzi ni aina gani ya kirusi. Aina hizo ni;-
•
Kirusi cha leafroll virusi (PLRV)
•
Kirusi cha S (PVS)
•
Kirusi cha X (PVX)
•
Kirusi cha Y (PVY)
•
Kirusi cha M (PVM)
•
Kirusi cha A (PVA)
Jinsi
ya kudhibiti magonjwa ya virusi:
• Kwa kutumia mbegu zilizosafi na bora.
Ni hatari sana kwa mkulima kuendelea kuchagua viazi vya mbegu kulingana na
ukubwa peke yake, mara nyingi mimea aliyoambukizwa na magonjwa ya virusi kwa
ujumla huzalisha viazi vya saizi ndogo ndogo.
• Kung’oa na kutaketaza mimea yote
aliyoambukizwa na magonjwa ya virusi: Kwa wakulima wazalishaji wa mbegu,
wanashauriwa kuchunguza mashamba yao, na kuhakikisha wanaondoa na kuteketeza
mimea yote inayoonesha dalili za magonjwa ya virusi. Hii husaidia kwani virusi
vingine husambaa kwa njia ya wadudu kama vila wadudu mafuta.
• Kudhibiti wadudu ambayo wanaweza
kueneza magonjwa ya virusi: Kwa ujumla, wadudu kama vile wadudu mafuta, thrips,
na inzi weupe.
• Kwa kutumia mbegu za viazi zenye
ukinzania wa magonjwa ya virusi.
KUMBUKA:
Virusi haviwezi kudhibitiwa na aina yoyote ya madawa ya kuulia wadudu.
Virusi
aina ya Leafroll (PLRV)
Ugonjwa huu ni muhimu katika mimea viazi
mviringo, na unaweza kusababisha mavuno kupunguzwa hadi kufikia 80%.
DALILI
Majani kujikunja kwa kwenda juu na
kugeuka rangi ya njano. Kama ukiyagusa huwa yanatoa sauti kama majani
yaliyokauka, kisha huwa yanavunjika vunjika. Maambukizi yakizidi husababisha
mimea ya viazi huzaa viazi vidogo vidogo, au kutotoa viazi vyovyote.
Jinsi
ugonjwa unavyoambukizwa
Virusi hivi vinaweza kuletwa ndani ya
viazi au shambani na viazi vya mbegu vilivyoambukizwa au kwa kutumia wadudu
mafuta ambao hueneza ugonjwa kutoka shamba moja hadi jingine.
Virusi
aina ya PVY
Aina hii ni ya pili kwa umuhimu. Ni
ugonjwa unaoweza kuambukizwa kupitia mbegu zilizoathrika au kwa njia ya wadudu
mafuta na virusi hawa wanaweza kupunguza mavuno kwa 90%.
DALILI
ZA UGONJWA
Majani ya mimea hukauka na
kupasukapasuka, pia michirizi ya majani huwa ya rangi ya manjano.
Japo kuwa ugonja huu unaweza kuambukizwa
kutoka kwenye mbegu zilizoathrika na baadhi ya zana za kilimo zitumikazo
shambani, pia ugonjwa huu unaambukizwa sana na wadudu mafuta ambao huweza
kufyoza vimelea vya ugonjwa kutoka mmea mmoja na kupeleka mmea mwingine ndani
ya muda mfupi.
Ugonjwa
wa Minyoo fundo au Viwavi (Root-knot nematode)
Huu ni ugonjwa ambao huharibu sana
sehemu za chini ya mimea, hasa viazi vyenyewe pamoja na mizizi ya viazi. Ingawa
ugonjwa huu unapatikana katika maeneo mengi yanayolimwa viazi, lakini wakulima
huona kama sio ugonjwa wa kutisha, hivyo kutoudhibiti.
Hata hivyo, viwavi hawa wanaweza
kupunguza ubora wa mbegu kwa wakulima wanaojishughulisha na ulimaji wa mbegu za
viazi mviringo. Vidonda vinavyosababishwa na viwavi hawa huweza kutoa mwanya wa
maambukizi ya magonjwa mengine, hata kupelekea viazi kuanza kuoza.
DALILI
ZA UGONJWA
Magonjwa yanayosababishwa na viwavi hawa
hutofautiana, lakini dalili za kawaida za minyoo fundo ni:
• Kuvimba kwa viazi, na viwavi hao
husababisha kiazi kuwa na maupele yenye kutoa maji maji endapo vikiminywa na
kidole.
Jinsi
ugonjwa unavyoambukizwa
Vyanzo vya magonjwa haya ni kupitia
udongo uliokwishaathirika na mbegu zilizo na viwavi tayari. Viwavi vinaweza
kuzunguka katika udongo kwa msaada wa maji.
Jinsi
ya kudhibiti ugonjwa
Viwavi vinaweza kudhibitiwa kwa kufanya
yafuatayo:
• Kwa kutumia mbegu zisizokuwa na
ugonjwa.
• Kutumia kilimo mzunguko wa mazao kwa
mfano mahindi au mazao mengine yasiyo jamii ya viazi.
• Kupulizia dawa maalum ya kuuwa viwavi
ndani ya udongo
UPUNGUFU
WA MADINI
Ishara
ya ukosefu wa virutubisho ni:
• Nitrogen:
1.
Njano njano ya majani.
2.
Kudumaa ukuaji wa mimea.
• Phosphorus:
1.
Mimea kuwa mifupi
2.
Majani kugeuka rangi ya kijani na
kujikunja kwa kwenda juu.
·
Potassium:
1.
Mimea kudumaa, majani kuonekana meusi.
• Calcium:
1.
Mashina kukausha
2.
Majani madogo kujikunja.
No comments:
Post a Comment