Monday, 13 March 2017

KILIMO CHA VIAZI MVIRINGO KINAENDELEA

JINSI YA KUANDAA MBEGU BORA YA VIAZI MVIRINGO
Wakulima wengi wamezoea kuandaa mbegu zao za viazi kwa kuchambua mbegu hizo mara tu baada ya kuvuna. Uchambuzi hufanyika kwa kuangalia zile ndogondogo na kuzihifadhi kwa ajili ya msimu unaofuata. Pia kuna wakulima wengine ambao hutegemea kupata au kununua mbegu kutoka kwa wakulima wengine walio jirani au kwenda sehemu fulani kununua mbegu za
viazi. Hali hii kitaalam haishauriwi, kwani kununua mbegu kwa mkulima bila kujua usalama wa mbegu hizo, ni hatari sana, kwani hupelekea mkulima kuuziwa mbegu zenye magonjwa au wadudu. Kwa kufanya hivyo pia huweza kuambukiza magonjwa na wadudu kutoka shamba moja na linguine.  Mkulima anashauriwa kununua mbegu bora kutoka kwa wakulima waliosajiliwa kwa ajili ya kuzalisha mbegu, na kuziuza kwa wakulima wa viazi vya chakula. Vile vile mkulima anaweza kununua mbegu kutoka kwa makampuni yanayojishughulisha na uzalishaji wa mbegu za viazi mviringo.
TEKNOLOJIA YA KUZALISHA MBEGU ZA VIAZI MVIRINGO
Wakulima wengi hawana uwezo wa kununua mbegu za viazi kutoka kwa makampuni yanayozalisha mbegu za viazi, kila mara. Kwa kutambua hilo, wakulima wanashauriwa kutumia teknolojia yakuzalisha mbegu kutoka kwenye mashamba yao ya viazi vya chakula. Zipo teknolojia za aina mbili ambazo mkulima anashauriwa kuzitumia kwenye kuzalisha mbegu zake kwa matumizi yake mwenyewe. Mbegu zinazozalisha kwa njia hizo, mkulima haruhusiwi kuziuza kwani ni mbegu ambazo hazijakaguliwa na wataalam. Teknolojia hizi zinaruhusiwa kwa wakulima wanaozalisha mbegu kwa matumizi yao binafsi.
1.      TEKNOLOJIA YA CHAGUA ILIYO BORA (Positive selection)
Hii ni teknolojia ambayo inamtaka mkulima kuchagua mimea iliyo bora kutoka shambani kwake, kisha na kuiwekea alama na kuanza kuihudumia vizuri kwa kuichunguza bila kuruhusu magonjwa na wadudu. Mimea hiyo huvunwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya mbegu msimu unaofuata. Njia hii ni rahisi na isiyokuwa na gharama, kwani mkulima hutumia mbegu zake mwenyewe na Shamba Lake, kuandaa mbegu za viazi. Kama mkulima atafuata maelekezo ya kitaalam jinsi ya kuchagua mimea na kuihudumia utafiti unaonesha mkulima hupata mbegu iliyo bora sawa au karibia na sawa na mbegu zinazozalishwa na wakulima waliosajiliwa.
2.      Teknolojia ya chagua isiyo bora (Negative selection)
Hii ni teknolojia ambayo hutumiwa na wakulima hasa wale waliotenga sehemu au shamba kwa ajili ya kuzalisha mbegu kwa matumizi yao. Njia hii inamruhusu mkulima kuchunguza ndani ya shamba lake la mbegu, kisha kung’oa mimea yote yenye kuonesha udhahifu wa magonjwa au wadudu. Mimea yote inayong’olewa huteketezwa kwa kuchomwa moto, ili isiendelee kuambukiza ugonjwa kwa mingine ndani ya shamba. Baada ya kufanya uchambuzi huo, mimea inayobaki shambani hutunzwa vizuri hadi kufikia kuvunwa, kisha na kuhifadhiwa tayari kwa kutumika kama mbegu msimu unaofuata.
Matumizi ya Mbolea
Viazi mviringo ni moja kati ya mazao yanoyotumia mbolea au virutubisho vingi shambani. Udongo huwa una aina mbalimbali za virutubisho, ambavyo vinahitajka kwa mmea kuweza kustawi. Hata hivyo virutubisho hivyo hupungua msimu hadi msimu kulingana na mazao yanayolimwa shambani. Kilimo cha viazi hutumia sana virutubisho, hivyo mkulima anatakiwa uchunguza na kujua ni aina gani ya virutubisho vimepungua kwenye udongo, ili aweze kuongeza virutubisho kupitia mbolea za viwandani au mbolea za asili.Mkulima anashauriwa kutumia mbolea ya asili au mbolea ya viwandani. Kama mkulima anao uwezo wa kutumia mbolea ya asili kama Mboji, au mbolea ya wanyama kama ng’ombe, ni vizuri kwani mbolea hii huongeza na kutunza afya ya udongo mara itumiwapo. Mbolea ya ng’ombe mkulima anashauriwa kutumia tani 7 kwenye hekita moja, na hii inatakiwa iwekwe kabla ya mvua kunyesha na kabla ya kupanda. Mbolea hii hufanya kazi polepole, hivyo kutoleta matokeo kwa mmea kwa haraka.
Mbolea za viwandani hutumika katika kilimo cha viazi.Mbolea hii hupatikana madukani. Kwa upande wa viazi mviringo mkulima anashauriwa kutumia mbolea ya kupandia na kukuzia ili kupata mavuno yenye tija. Mfano wa mbolea za kupandia ni kama DAP, TSP, na NPK. Mbolea za kukuzia ni kama CAN au wakati mwingine mkulima anaweza kutumia SA. Mbolea ya NPK yenye uwiano wa 17:17:17, inafaa sana kwa kilimo cha viazi mvringo. Mbolea hii ni nzuri kutokana na kwamba ina virutubisho vikubwa vitatu kwa pamoja vinavyohitajika kwenye mmea wa viazi. Pia faida nyingine ya kutumia mbolea ya NPK ni kwamba huhitaji kuweka tena mbolea ya kukuzia.
KILIMO MZUNGUKO WA MAZAO
Kilimo mzunguko wa mazao ni jambo muhimu sana kwa wakulima wa viazi, hasa wale wazalishaji wa mbegu. Kilimo mzunguko kina faida nyingi sana kwa mkulima wa viazi. Kwa kawaida wakati wa kuvuna mkulima hawezi kumaliza viazi vyote shambani, hali huchangia hata kuwa na magonjwa  na wadudu shambani, iwapo viazi vilivyo bakia shambani vitakuwa na magonjwa na wadudu. Ili kupunguza maambukizi, mkulima anashauriwa kuhakikisha mabaki yote yanatolewa. Njia nzuri ya kufanya ni kuwa na mzunguko wa mazao., kwani hii itasaidia kuondoa mabaki ya viazi hasa kipindi cha palizi la zao husika. Kilimo mzunguko kina faida kama; kuepuka kuongezeka kwa magonjwa na wadudu wanaopendelea kuishi na kula kwenye zao la viazi, husaidia kuongeza rutuba ndani ya shamba, na pia mkulima hupata zao linguine la kumletea chakula au pesa za kujikimu hasa kipindi cha msimu usiokuwa wa viazi.

MAMBO YA KUFANYA KABLA, WAKATI NA BAADA YA KUVUNA VIAZI
Viazi vinachukua muda wa siku 90 mpaka 120 kukomaa, tangu kupandwa. Mkulima anashauriwa kufahamu ni muda gani anatakiwa kufanya maandalizi ya kuvuna. Kuna mambo ambayo mkulima anapaswa kufanyakama maandalizi ya kuvuna. Mambo hayo ni kama; kukata mashina ya viazi mara ifikapo siku ya 80 mpaka 85 kabla ya kuvunwa. Kufanya hivyo husaidia kukomaa kwa ngozi ya viazi ili vinapovunwa visipate michubuko inayoweza kusaidia kuingiza maginjwa na wadudu ndania ya mbegu.  Pia kukata kwa mashina husaidia viazi vya mbegu kuwa na ukubwa sawa au karibia na sawa, hii ni muhimu kwa wazalishaji wa mbegu.
WAKATI WA KUVUNA
Zoezi la kuvuna viazi mviringo ni hatua ya mwisho ya kuondoa viazi kutoka shambani. Wakulima wengi hutumia jembe la mkono wakati wa kuvuna, na wakulima wachache hutumia jembe la kukokotwa na ng’ombe. Ni wakulima wachache sana wanaotumia mashine maalum ya kuvunia viazi. Mambo ya kuzingatia wakati wa kuvuna viazi;
1.      Hakikisha mashina yote yamekatwa wiki 3 kabla ya kuvuna
2.      Anza kuvuna kipindi cha kiangazi, kisichokuwa na mvua
3.      Hakikisha wakati wa kuvuna viazi visipate michubuko ya aina yoyote
4.      Hakikisha viazi vilivyovunwa havina unyevunyevu kabla ya kuvihifadhi kwenye ghala
5.      Chambua viazi vyote vilivyo katika kabla ya kupeleka ghalani
6.      Hakikisha ghala lako ni safi na limepuliziwa dawa za kuulia wadudu
7.      Weka viazi vyako kwenye kichanja ndani ya ghala.

JINSI YA KUHIFADHI VIAZI MVIRINGO
Viazi mviringo kama ilivyo kwa mazao mengine, huhitaji kuhifadhiwa mara tu baada ya kuvunwa. Lakini kwa upande wa viazi mvringo, jinsi ya kuhifadhi ni tofauti na mazao mengine. Viazi vinapovuna huwa kwenye hali ya uhai, na hali hiyo inatakiwa kutunzwa mpaka wakati wa kupanda kwa upande wa mbegu. Kutokana na asili ya viazi mviringo, mkulima anashauriwa kuwa na sehemu maalum au gahala nzuri la kuhifadhia mbegu za viazi mviringo.

SIFA ZA GHALA LA VIAZI MVIRINGO
1.      Liwe na linaloruhusu mwanga na hewa
2.      Liwe na neti inayozuia wadudu kuingia na kuharibu mbegu
3.      Liwe limewekewa vichanja kwa ajili ya kuwekea mbegu
4.      Liwe limeezekwa vizuri ili kuzuia maji ya mvua kuingia

5.      Liwe na mlango mpana wa kuweza kupitisha gunia la mbegu au troli kupita.

4 comments:

  1. nini maana ya kilimo mzunguko?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kilimo mzunguko ni kilimo cha kubadirisha mazao mwaka kwa mwaka mfano mwaka huu umelima viazi mviringo mwakani unalima hata mahindi iko hivyo

      Delete
  2. Ni sahihi kuanika viazi juani vilivyochambuliwa kwa ajili ya mbegu kabla kuhifadhi ghalan?

    ReplyDelete
  3. Cool and I have a super provide: Who Repairs House Siding split level house exterior remodel

    ReplyDelete