Monday, 13 March 2017

UFUGAJI WA SAMAKI

UFUGAJI WA SAMAKI

UTANGULIZI

Ufugaji wa samaki unahusisha kuwafuga samaki katika mazingira tengefu (yasiyo ya asili kwenye mabwawa au matangi) na kuwavuna kwa aajili ya kula katika familia au kuwauza sokoni.

Historia ya ufugaji
wa viumbe-maji inaonekana kuwepo tangu enzi za zamani sana. Katika maandishi ya mkono yaliyoandikwa na Wachina wa kale karne ya 5 kabla ya Kristo yanaonyesha kuwa Wachina walikuwa wanafuga samaki. Historia pia inaonyesha kuwa ufugaji mkubwa ulijaribiwa na Wamisri wakati wa Ufalme wa kati (2052-1786 kabla ya Kristo) japo hauonyeshi kama walifanikiwa na ufugaji huo. Ufugaji aina ya Kombe ulifuatiwa na Warumi ambao kumbukumbu zake ziliwekwa vizuri na umeendelezwa katika njia tofauti hata katika nyakati za sasa.Njia nyingi za ufugaji wa samaki za zamani inatofautiana sana na njia tunazoziona leo hii na tofauti kubwa ni kwamba zamani waliwavua samaki wadogo toka mazingira asili na kuwahamishia katika mazingira yaliyotengenezwa kwa kufugia.

Ufugaji wa huu wa kisasa ulianza kutumiwa mnamo mwaka 1733 pale ambapo mkulima wa Kijermani alipofanikiwa kukusanya mayai ya samaki, akayarutubisha na kuyaangua kisha samaki hawa watoto wakapelekwa kwenye matangi au mabwawa ya kufugia samaki. Mwanzoni ufugaji huu ulifanyika kwenye maji baridi na samaki wa maji baridi na baadaye karne ya 20 hivi ufugaji wa maji-chumvi kwa kutumia samaki wa maji-chumvi ulianza kwa vile ujuzi mpya ulikuwa umegunduliwa.

Historia ya ufugaji wa samaki Tanzania haujawekwa vizuri kwenye maandishi, lakini kulingana na Balarin (1985) anasema majaribio yalianza mnamo mwaka 1949 katika mikoa ya Tanga (Korogwe) na Mwanza (Maly) ikionyesha kujengwa pia kwa mabwawa mengi ya samaki. Lakini mabwawa haya yaliishia kutofanya kazi kwasababu ya kukosa usimamiaji mzuri, matumizi ya technolojia isiyosahihi pamoja na matatizo mengine kama ya ukame na miundo mbinu mibovu. Kulingana na ripoti iliyotolewa na FAO mwaka 1968 ilionyesha kuwa Tanzania ilikuwa na mabwawa 8000 ya kufugia samaki japo mengine yalikuwa madogo yenye uzalishaji kidogo kulingana pengine na usimamizi mbovu.

Mwaka 1967 serikali ya Tanzania ilianzisha kampeni ya kuhamasisha ufugaji wa samaki, lakini ilishindikana kwasababu ya mipango mibovu na usimamizi mbovu. Mwaka 1972 kwa mara ya kwanza ufugaji wa samaki ulipewa umuhimu kisera japo sheria ilitungwa mwaka 1970. Mwaka 1997 sera ya ufugaji wa samaki ilipitishwa iliyoipa kipaombele ufugaji wa samaki.

Ufugaji wa samaki Tanzania kwa sehemu kubwa unafanywa kama kazi ya ziada na wafugaji 17100 wanafanya ufugaji wa maji baridi na 3 000 wa maji chumvi. Kuna takribani mabwawa 14100 yaliyo maeneo mbalimbali ya nchi yetu na wafugaji wengi wa wale wafugaji wadogo wenye mabwawa yenye ukubwa wa mita za mraba 150. Mgawanyo wa mabwawa katika nchi yetu unategemea sana vitu vifuatavyo; upatikanaji wa maji, ardhi inayofaa kwa ufugaji wa samaki, uelewa na uhamasikaji wa jamii ukitegemeana na umuhimu kiuchumi wa ufugaji wa samaki. Kuna maeneo manne Tanzania ambako ufugaji wa samaki umeshamiri kwa kiasi fulani (una mabwawa yanayozidi 1000), nayo ni Ruvuma (4942), Iringa (3137), Mbeya (1176) na Kilimanjaro (1660). Mbali na kwamba kuna aina nyingi sana za samaki wanaofugwa duniani, lakini katika nchi yetu ya Tanzania ni aina kuu mbili zinazofugwa ambazo ni pelage au tilapia na kambale. Chaguo hili la wafugaji wengi wa aina hizi limetokana na urahisi wa kuwafuga hawa samaki kwa vile mahitaji yao si makubwa sana.

Kwa nini Mtanzania ufuge samaki?

Kuna upungufu mkubwa sana wa protini duniani na hasa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania inayotokana kwa asilimia kubwa na vyakula vya aina ya nyama. Upungufu huu wa protini ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya kiafya ya binadamu hasa watoto wadogo na vijana wa umri chini ya miaka 25 ambao wanahitaji kukuwa kwa haraka. Ugonjwa wa Kwashako kwa watoto ndiyo matokeo ya upungufu wa protini mwilini.

Pia matumizi ya samaki na hasa mafuta ya samaki ambayo ndo yanatumika sana kuwanywesha watoto wadogo yamethibitika kisayansi kuwa yanasaidia sana ukuaji wa ubongo wa mwanadamu. Lakini pia uwepo wa kiwango kidogo sana cha kolestero ambayo imeripotiwa kusababisha ugonjwa wa moyo kimepelekea ongezeko la watu wanakula samaki.

Sababu zifuatazo hapa chini zinatoa jibu la kwa nini Mtanzania ufuge samaki;
-Ongezeko kubwa la uhitaji wa samaki ndani na nje ya nchi yetu kunakofanya samaki waliopa sasa kutotosheleza mahitaji.
-Kupungua kwa samaki asili kwenye mito, maziwa na bahari kunakotokana na uvuvi wa kupindukia na haramu.
-Urahisi wa kufuga samaki kwa vile hawahitaji eneo kubwa na chakula kisichokuwa na gharama kubwa.
-Wanauwezo wa kutoa mazao mengi(faida kubwa) katika eneo dogo tena ndani ya muda mfupi (uvunaji huanza baada ya miezi mitatu au mine hivi na uvunaji wa mwisho kati ya miezi 6 hadi 12).
-Ufugaji wa samaki utasaidia familia kupata kitoweo pasipo gharama za ziada na tena utapata protini ya uhakika.
-Upatikanaji wa maji maeneo mengi ya nchi yetu hasa angalau kwa muda miezi michache kwa mwaka kiasi cha kutoa fursa ya kuzalisha samaki katika kipindi ambacho maji yanakuwepo. Lakini pia maeneo yenye maji ya bomba yanaweza kuzalisha samaki muda wote wowote.
-Samaki wanavumilia sana magonjwa, hata mazingira duni wanauwezo wa kuishi
-Ardhi tuliyonayo maeneo mengi ya Tanzania inakidhi ufugaji wa samaki
Tatizo la kuwa kuwa na ufugaji mdogo wa samaki unachangiwa kwa kiasi kikubwa uduni wa elimu ya ufugaji wa samaki katika maeneo mengi. Maeneo ambayo elimu ya kutosha imetolewa watu wengi wamenufaika na ufugaji wa samaki na ufugaji umeshamiri kwa kiasi fulani. Ufugaji wa samaki hauhitaji rasilimali nyingi au zilizo nje ya uwezo wa mwanchi wa kawaida wa Tanzania. Mahitaji ya samaki mengi yanapatikana katika maeneo anayoishi mwananchi na wala hauhitaji muda mwingi kiasi cha kuathiri kazi nyingine.

Kama ilivyo kwa mifugo mingine yeyote ile, kabla ya kuanza ufugaji kuna mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa ili ufugaji wako uweze kuwa na tija iliyokusudiwa. Mambo hayo ni kama ifuatavyo:
1. Chagua mbegu bora ya samaki unaotaka kuwafuga ili wakuletee mazao bora na mengi
2. Samaki wapewe makazi bora yatakayo msitiri dhidi ya hali mbaya ya hewa kama joto, baridi n.k yaliyo safi wakati wowote ili kuepusha magonjwa.
3. Hakikisha samaki wanapewa chakula chenye viini lishe vinavyohitajika na kiwe cha kutosha ili waweze kukua na kuzaliana kwa wingi na uwauze kwa wakati.
3. Hakikisha samaki wagonjwa wanapewa tiba kwa wakati ili usisambae kwa wengine lakini pia yeye mwenyewe asidhoofike na kufa.
4. Chagua eneo zuri linalofaa ufugaji kwa kuangalia upatikanaji wa maji ya kutosha, aina ya udongo, mwinuko na liwe karibu na nyumbani kwako.
5. Angalia uhitaji wa soko katika eneo husika kama unapanga kufuga kibiashara

NAMNA YA KUANZA UFUGAJI

Ufugaji unaanza na utengenezaji wa eneo la kufugia samaki yaani bwawa au tanki kutegemeana eneo ulilo nalo. Hapa nitongelea mambo muhimu ya kuangalia kama unataka kufuga samaki kwenye bwawa na mabwawa mengi nchini yale ya udongo. Mambo muhimu ya kuangalia wakati unaangalia eneo la kujenga bwawa la samaki ni eneo la ardhi lilivyo, upatkanaji wa maji na aina ya udongo.

1. Eneo la ardhi

Hakikisha eneo la ardhi ni tambalare na mwinuko kidogo unaruhusiwa, lakini eneo hilo lisiruhusu kuwepo kwa mafuriko. Ukubwa wa eneo utategemea na kiasi cha samaki unaotarajia kuwafuga. Hakikisha kuwa eneo hilo halina aina yeyote ile ya uchafuzi wa mazingira, lisiwe na miti mingi na vichaka vitakavyozuia jua na mwanga.

2. Upatikanaji wa maji

Maji ndo mazingira yanayomfanya samaki aishi kwani upumuaji wake (kutumia matamvua) unategemea kwa asilimia 100 uwepo wa maji, nje ya maji hishi dakika kadhaa tu kabla ya kupoteza uhai wake.  Hivyo eneo la kufugia lazima liwe na maji ya kutosha na salama kwa kipindi cha mwaka mzima. Vyanzo vya maji kwa ajili ya ufugaji wa samaki ni kama chemichemi, mito, maziwa na maji ya ardhini (visima). Hakikisha vyanzo vya maji ni salama kwa maana kuwa kusiwe na madawa yanayoweza kuathiri samaki mfano madawa ya kupulizia nyanya au mbogamboga. Maji yaliyo ndani ya bwawa yanapaswa kuwa na joto kwa kiasi fulani kwani ni muhimu sana kwa ukuaji wa samaki. Tilapia anakuwa vizuri katika maji yenye uvuguvugu (nyuzi joto 25-30) katika nyanda za chini lakini anaweza kuishi katika maji ya baridi sehemu za mwinuko akikkua taratibu na kuzaliana polepole.

3. Aina ya udongo

Maeneo yenye udongo wa mfinyanzi yanafaa sana kuchimba mabwawa ya kufugia samaki. Udongo mzuri unatakiwa usiwe na changarawe, mawe wala usiwe na mchanga mwingi kwani hautakuwa na uwezo wa kutuamisha maji kwa muda mrefu. Eneo lenye udongo kama ule unaotumika kutengenezea vyungu na kufyatulia matofali ndo mzuri sana kwa kwa kujenga bwawa la samaki.


4. Mambo mengine ya kuangalia wakati wa kuchagua eneo la ujenzi wa bwawa

a) Ukaribu na soko la samaki:

Bwawa ni vema likajengwa karibu na soko la samaki lilipo la sivyo kuwepo na miundo mbinu ya uhakika ya kuwafisha hao samaki sokoni bila kuharibika. Hasa hii itakuwa muhimu sana endapo unakusudia kufanya ufugaji mkubwa na itapunguza uharibikaji wa samaki wakati wa kuvua.

b) Upatikanaji wa pembejeo:

Upatikanaji wa vifaranga katika eneo la karibu ni vizuri ili kupunguza vifo vya mbegu hizo za samaki wakati wa kusafirisha. Pembejeo nyingine ni pamoja na upatikanaji wa mbolea (samadi na ya kiwandani) lazima vizingatiwe kwani ni muhimu kwa urutubishaji wa bwawa wakati unatengeneza chakula cha samaki.

c) Miundo mbinu:

Hakikisha miundo mbinu ya mawasiliano inapatikana mfano simu, barabara, na umeme hasa kama unakusudia kufanya ufugaji mkubwa. Hivi vitakusadia sana kujua soko na kuwafikisha samaki sokoni kwa wakati wakati wanapohitajika. 

d) Wafanyakazi:

Ufugaji mkubwa unahitaji msaada wa watu wengine wa kukusaidia kufanya kazi kwenye shamba lako la samaki. Tumia watu wenye ujuzi wa kufuga samaki, wenye kujituma kufanya kazi hiyo na ikiwezekana wapelekwe kozi ili wawe msaada mkubwa kwako na kazi ifanywe kwa ustadi.

e) Ushauri wa kiufundi:

Kama wewe si mtaalamu na wakati mwingine kama ni mtaalamu hakikisha kwamba unauwezo wa kupata ushauri pale utakapo hitaji. Ushauri unaweza kuupata toka kwa wafugaji wenzako wa samaki au hata kwa maafisa wa samaki walipo katika eneo husika. Lakini kwa utandawazi wa sasa ushauri unaweza kuupata toka hata kwa mtu aliye mbali. Thibitisha ushauri unaopewa kwa watu zaidi ya mmoja ili kujiridhisha.

f) Ushindani:

Ni vema kujua washindani wako katika ufugaji na nguvu waliyonayo kibiashara katika eneo lako. Hii itakusaidia kujua kama ufugaji wako utakuwa na manufaa kwako na hasa kama umekusudia uwe wa kibiashara.

g) Maswala ya Kisheria:

 Ni vema kujiridhisha kama kunasheria inayozuia kufanya ufugaji wa samaki katika eneo husika ili isije kukuletea matatizo baadaye. Angalia sheria ya ufugaji wa samaki, sheria ya ardhi, sheria ya maji na sheria ya mazingira zinasemaje juu ya ufugaji wa samaki katika eneo kama hilo unalokusudia kufugia samaki.
Baada ya kujiridhisha na mambo yote hapo juu sasa unaweza kuendelea na mipangilio ya ujenzi wa bwawa.

5. Aina ya mabwawa ya kufugia samaki

Mabwawa yote yanayotumika kufugia samaki yanaangukia katika aina kuu tatu na uchaguzi wa aina ya bwawa lipi litumike wapi inategemea sana mwonekano au sura ya ardhi litakapokuwa bwawa hilo. Aina zenyewe kama ifuatavyo:

Mabwawa ya kukinga mto:

Mabwawa haya yanatengenezwa kwa kujenga ukuta utakaowezesha maji kusimama kwa kukinga mto au kijito kwa ajili ya ufugaji wa samaki. Mifereji ya kuchepusha mto hujengwa ili kuruhusu maji yapungue pale yanapokuwa mengi na mengine huwekewa chujio sehemu ya kutolea maji katika ule usawa unahitajika ili maji yakifika pale yatoke bila kutoka na samaki.

 Mabwawa haya huchimbwa katika nchi yenye uwanda wa tambarale lakini yenye chemichemi za maji yanayobubujika kutoka ardhini ili bwawa likichimbwa yaweze kujikusanya ndani ya bwawa tayari kwa ufugaji wa samaki. Wakati wa kuvuna samaki si rahisi kuondoa maji hadi ukingo wa bwawa ubomolewe ili kuruhusu maji yatoke.
Kuna maeneo ambayo ardhi yake ni ya mwinuko na hivyo mabwawa ya aina hii hutumika kufugia samaki. Lakini pia aina hii ya mabwawa hujengwa hata mahali ambapo si pa mteremko ila kwa chini sakafu yake huwa ya mwinuko. Maji huingia na kutoka kwenye bwawa kwa njia ya mifereji au bomba. Na hii ndiyo aina ya mabwawa inayotumika na watu wengi kufugia samaki.

6. Aina ya mifumo ya ufugaji samaki

Ipo mifumo ya aina mbili; ya maji yaliyotuama ambao maji yakishajazwa ndani ya bwawa hukaa humo kwa muda mrefu bila kutolewa na mfumo wa maji yanayotembea ambapo maji huruhusiwa kuingia na kutoka bwawani wakati wote. Mfumo huu wa pili tofauti na wa kwanza mfugaji hawezi kurutubisha bwawa kwani virutubisho vitachukuliwa na maji na hvivyo ni wa gharama kubwa kwani unategemea chakula achowalisha samaki kila siku.

7. Aina ya samaki wanofugwa


Zipo aina nyingi sana za samaki wanaofugwa duniani, lakini kwasabau ya urahisi wa kufuga na gharama kidogo za ufugaji ambazo mfugaji wa kawaida anaweza kuzimudi, Tanzania kuna aina kuu mbili tu zinazofugwa na watu wengi. Ambazo ni perege (tilapia) na kambare (Catfish) ambao mahitaji yao si makubwa sana ukilinganisha na samaki wengine.Perege yeye ni samaki wa maji moto lakini kwa asilimia kubwa anafugwa kwenye maji baridi, kambare yeye pia anafugwa zaidi katika maji baridi.
Tatizo la ufugaji wa perege kwenye mabwawa ni uzalianaji usiodhibitika wakati changamoto ya ufugaji wa kambare ni vifo vingi hasa siku 14 za mwanzo mara baada ya kuanguliwa kwa mayai. 

No comments:

Post a Comment