Perege:
Anakuwa vizuri katka maji yenye nyuzi joto kati ya 20 na 35
na anauwezo wa kukua hadi gramu 500 kwa ndani ya muda wa miezi 8 kama
uzalianaji wake ukidhibitiwa vizru na akapewa chakula cha kutosha. Perege
anaweza kupevuka (kubarehe) mapema akifikisha umri wa miezi 2 au akiwa na urefu
sm 10 au chini ya hapo, lakini kwa kawaida ni miezi 4 hadi 6. Mapungufu ya huyu
samaki ni kitendo cha kuzaliana kwa wingi ndani ya muda mfupi inayopeleke kuwa
na samaki wenye uzito mdogo kwa vile wamejazana sana ndani ya bwawa. Kwa vile
perege ni samaji wa maji joto, hivyo joto linatakiwa lisishuke chini ya
nyuzijoto 16, chini ya hapo samaki hawaendelei kukua na hasa linapofikia
nyuzijoto 13. Perege huanza kufa joto linapo shuka hadi nyuzi joto 12 na samaki
wachache sana watakao weza kuhimili joto chini ya nyuzi joto 10. Hivyo
hakikisha siku zote joto lipo kati ya nyuzi joto 20 na 30 na vizuri zaidi kama
linabaki nyuzi joto28. Joto pia likizidi zadi ya hapo litasababisha samaki
wafe.
Kambare:
Kwa kawaida kambare hupevuka
(hubalehe) wakiwa na umri wa miaka 2 wakiwa na uzito kati ya gramu 200 hadi
500. Majike wanauwezo wa kutaga mayai kati ya 10,000 hadi 15,000 kutegemeana na
ukubwa na umri wa samaki. Samaki hawa hukua vizuri maji yakiwa na nyuzi joto
kati 26-33, lakini kwa wastani nyuzi joto 28. Kambare wao hata joto likiwa
chini ya hapo bado hukua vizuri tofauti na perege.
RASIMU YA UTENGENEZAJI WA WA MABWAWA
Bwawa la samaki ni uzio/ukingo wa
udongo, zege au saruji uliotengenezwa kubakisha maji kwa ajili ya ufugaji wa
samaki. Vihori vya miti au matanki ya plastiki ni vitu vingine vinavyoweza
kutumika kwa ufugaji wa samaki.
Mambo muhimu ya kuzingatia
1. Vyanzo vya maji vitakavyotumika kwenye bwawa la samaki
Vyanzo vya maji vinaweza kuwa
chemichemi, visima, chururu, maji ya mvua, maji mito, maji ya bomba na maji ya
ziwa. Uwingi wa maji utategemea na ukubwa wa bwawa au ukubwa wa mradi unaofuga.
Maji haya lazima yawe masafi yasiyo na wadudu wa magonjwa au wa kuua samaki.
2. Uletaji na utoaji wa maji kwenye bwawa
Hakikisha sehemu ya kuingizia maji
ipo juu zaidi ya ile ya kutolea angalau kwa tofauti ya mita moja na nusu. Panga
mshuko wa sentimita 10 kutoka maji yanapoingilia hadi usawa wa maji ilikuzuia
samaki wasiogelee na kutoka nje kupitia uwazi wa kupitia maji. Maji yanaweza
kujazwa kwenye bwawa kwa kutumia pampu pia lakini kama una chanzo rahisi epuka
matumizi ya pampu.
Sehemu ya kuingizia maji huwa upande
ule wenye kina kifupi na huwa juu kabisa ambapo usawa wa maji ndani ya bwawa
unapaswa kufika. Kama chanzo cha maji ni mto unatirika kwa kasi basi hakikisha
unajenga vizuri kwa zege sehemu maji yanapoingilia na weka nyavu za kuzuia
wadudu waharibifu wanaoweza kuja na maji. Kama chanzo ni maji ya bomba au
unapampu kutoka kwenye kisima basi si lazima sana uweke wavu. Na kwa wafugaji
wadogo hawahitaji kuwa na sehemu hii ya kuingizia maji hasa kama maji wanaweka
kwa kutumia ndoo.
Sehemu ya kutolea maji ya bwawa
inatakiwa iwe upande wa bwawa wenye kina kirefu ambako mteremko wa chini ya
bwawa unaelekea. Mara nyingi wafugaji wadogo wa samaki hawaweki mfumo huu wa
kutolea maji. Mfumo huu wa kutolea maji ni muhimu sana kwa ajili ya ukaushaji
wa bwawa mara baada ya kuvuna samaki wote ndani ya bwawa. Wakati wa uvunaji
unaweza kutoa maji yote au ukatoa kidogo kurahisiha uvunaji lakini kama unavuna
wote ni vema ukatoa maji yote, ukasafisha vizuri bwawa na kulikausha kabla
hujaweka samaki wengine. Utoaji kidogo au upunguzaji wa maji hufanyika pale
maji yanapozidi usawa unaotakiwa hasa wakati wa mvua. Maji yanapozidi usawa
unaotakiwa huwa hatari kwa bwawa kwani yatalidhoofisha na kusababisha kuta
zianze kuporomoka.
3. Ukubwa wa bwawa, umbile na kina chake
Ukubwa wa bwawa utategemea ukubwa wa
mradi wa samaki unaokusudia kuufanya na kama ni kibiashara au matumizi tu ya
nyumbani. Kama ni kwa matumizi ya nyumbani basi ukubwa wa bwawa usizidi eneo la
mita za mraba 1000. Lakini kama ni la ufugaji mdogo wa kibiashara eneo la mita
za mraba kati ya 2000 hadi 3000 zinaweza kumilikiwa kirahisi na familia.
Mabwawa ya msitari ndiyo rahisi
kuyajenga pamoja na kuyaendesha, lakini pia mabwawa yanaweza kuwa na umbile
lolote lile kutegemea eneo ulilonalo linavyoweza kutumika kujenga bwawa.
Kina cha bwawa kitategemea aina ya
samaki, ukubwa wa samaki na mfumo wa uzalianaji. Lakini bwawa la kawaida
linatakiwa liwe na kina kati ya mita 0.75 na 1.2. Upande wenye kina kifupi cha
bwawa unatakiwa uwe kati ya sentimita 40 hadi 70, lakini vizuri zaidi iwe kati
ya sentimita 50 na 60 kuepuka wanyama wala samaki (kama ndege) na magugu.
Upande wenye kina kirefu unafaa uwe kati ya sentimita 80 na 120 lakini kwa
mabwawa ya kati na makubwa inafaa kiwe kati ya sentimita 90 na 110.
Mabwawa madogo yenye eneo la mita za
mraba 150 kina kifupi kinapaswa kiwe sentimita 50. Kumbuka kuwa mwanga wa jua
unaweza kupenya hadi kina cha mita moja kwa mabwawa ambayo hayajawekwa mbolea
na yale yenye mbolea ni sentimita 60.
4. Mwinuko wa bwana chini
Bwawa linapaswa liwe na mwinuko
mzuri kwa ajili ya utoaji wa maji ndani ya bwawa. Kwa kawaida mwinuko unaoshuka
kwa sentimita 2 kila baada ya urefu wa mita 10 kwavusawa wa chini ya bwawa
unafaa sana. Kama mwinuko ukiwa mdogo sana utokaji wa maji utakuwa taratibu na
kama mwinuko ukiwa mkubwa sana, upande mmoja wa bwawa utakuwa na kina kirefu
wakati upande mwingine mfupi sana.
UTENGENEZAJI WA BWAWA.
Haya ni mabwawa yanayotengenezwa kwa kuchimba udongo kwa
umakini mkubwa sana katika eneo lililochaguliwa na kuonekana linafaa kwa
kutengeneza bwawa. Na kama eneo linaudongo unakunywa maji, basi bwawa
liwezeshwe kwa kumimina zege kufanya lifae kwa ufugaji wa samaki.
Haya ni mabwawa yanayotengenezwa ardhini kwa kwenda juu
yakiwa yametengenezwa kwa kuta za nzege, tofari za simenti na hata za udongo
zilizochomwa. Na maranyingi haya yanajengwa maeneo ambako udongo wake ni wa
mchanga, unafyonza maji sana au kwenye makazi ya watu na eneo ni dogo.
Hii ni aina ya mabwawa yanayotengenezwa kwa kujenga ukuta
unaozuia maji yanayotembea polepole kwenye bonde. Ukuta unaojengwa ni lazima
uwe na uwezo wa kuzuia maji kwa ajili ya ufugaji wa samaki.
Haya ni mabwawa
yanayopata maji yaliyochepushwa kutoka kwenye mto au maji yanayotembea kupitia
mfereji uliotengenezwa kwa kupitisha maji hayo kwenda bwawani.
Haya ni mabwawa
yanojengwa kwa mfuatano huku bwawa moja likilipekea bwawa jingine maji na yote
yanaendeshwa kwa pamoja kwasababu ya muunganikano wa maji. Kunakuwa na sehemu
moja ya kuingizia maji na moja ya kutolea maji.
Haya ni mabwawa yanokuwa yamejengwa kwa usambamba lakini
kila moja lina sehemu ya kuingizia maji nay a kutolea maji.
B. Utengenezaji wa mabwawa
Baada ya kuandaa rasimu ya bwawa
kinachofuata ni utengenezaji wa bwawa lenyewe kulingana na chaguo la aina ya
bwawa. Kuna mfuatano wa kimantiki wa kufuata wakati unatengeneza bwawa
kama ifuatavyo:
i) Kagua ardhi ya sehemu
unayokusudia kujenga bwawa ili ujue ni bwawa gani linafaa kujenga eneo husika.
ii) Safisha vizuri eneo husika,
fyeka kama kuna miti au majani
iii) Ondoa udongo wa juu kwenye eneo
iv) Tambua muonekano wa ardhi na
mwinuko kwa ajili ya mifereji ya kuingizia na kutolea maji.
v) Amua ukubwa wa bwawa unaoutaka
kisha pigilia vigingi (mambo) kwenye pembe litakamo ishia bwawa.
Uchimbaji wa bwawa
Uchimbaji wa bwawa waweza kufanywa
na watu kwa kutumia majembe ya mkono au kwa kutumia trekta/katapila hasa kama
bwawa unalokusudia kujenga ni kubwa sana. Hapa nitatumia mfano wa bwawa la mita
za mraba 200 (yaani urefu mita 20 na upana mita 10) ambalo latosha kwa samaki
kati ya 400 na 600. Baada ya kusafisha eneo fuata hatua zifuatazo:
i). Anza kwa kupima urefu wa mita 23
na upana wa mita 13 kwa kutumia kamba na mambo kama wafanyavyo wajenzi wa
nyumba.
ii) Kutengeneza umbo la mraba lenye
urefu wa mita 20 na upana wa mita 10, funga kamba kwenye pembe moja na ipeleke
kwenye pembe inayotazamana nayo, acha mita 2 kabla ya kufika hiyo pembe na piga
kigingi hapo. Fanya hivyo na kwa pembe nyingine mbili zinazobakia, utakuwa
umetengeneza umbo kama hili hapa chini.
iii) Anza sasa kuchimba bwawa kwa
kufuata mistari ya mstatiri ya ndani huku ukirusha udongo nje ya mstari wa nje
hadi kitakapofikia kina cha mita moja na sentimita 60 (m 1.60).
iv) Utengenezaji wa kuta za ukingo:
Hii ni sehemu ya muhimu sana katika bwawa na hutengenezwa kwa kutumia udongo
uliochimbwa kutoka kwenye bwawa. Kuta za bwawa huchongwa kwa kuanzia kwenye
mistari ya nje ili kupata kuta zenye mteremko.
iv) Utengenezaji wa sehemu za
kutolea maji: Tengeneza sehemu ya kutolea maji sehemu yenye kina kirefu kwa
kutmia bomba au waweza kutengeneza uwazi kwa kusakafia na sement na sehemu ya
kuingizia maji pia. Lakini kwa mabwawa madogo sehemu hizi zinaweza zisiwepo
kwani maji yanaweza kuingizwa kwa kutumia ndoo au mipira iliyounganishwa kwenye
bomba.
v) Urutubishaji awali: Tafuta udongo
mzuri wenye rutuba toka mashambani kisha usambaze juu ya sakafu ya bwawa hadi
kina cha sentimita 10 hivi ili kusaidia kurubisha bwawa kwa matumizi ya samaki.
vi) Uingizaji maji: Sasa bwawa liko
tayari kwa kuingiza maji ndani na ingiza kufikia kina cha mita moja hadi mita
moja na sentimita 20.
UINGIZAJI VIFARANGA
A) Uandaaji wa bwawa kabla ya kuingiza vifaranga
i) Bwawa jipya:
Bwawa linatakiwa lirutubishwe ili
kutengeneza chakula cha asili cha samaki kinachoitwa planktoni. Planktoni ni
mchanganyiko wa mimea na wanyama wadogo sana ambao hawaonekani kwa macho.
Urutubishaji wa aina hii hufanywa kwa kutumia molea ya samadi, mboji au
kiwandani na itategemea ipi inapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu. Mara
nyingi mbolea za asili(mbolea ya ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku, punda, sungura,
na mboji) zimeonekana kutumika zaidi kwa sababu ya upatikanji wake na bei yake
kuwa rahisi.
Njia zinazotumika kurubisha bwawa ni
pamoja na kusambaza mbolea kwenye bwawa kabla ya kujaza maji, kurushia mbolea
kila baada ya wiki moja juu ya maji na kuweka mbolea katika kihori (crib)
kinachojengwa kwa kutumia fito za miti au mianzi au kapu la kutengenezea mboji
vinavyowekwa kaitka moja ya kona upande wenye kina kifupi cha maji. Njia
nyingine ni pamoja na kuweka gunia lililojaa mbolea na kuliacha lielee juu ya
maji, tikisa kila siku ili virutubisho viangukie kwenye maji. Pia waweza
kujenga banda la kuku au nguruwe juu au karibu na bwawa katika njia
itayowezesha mbolea iende kwenye bwawa.
Bwawa litaanza kuonyesha mabadiliko
baada ya wiki moja ambapo maji yataanza kubadilika na kuwa na rangi ya kijani au kahawia.
Ukitumbukiza mkono wako ndani ya maji hadi usawa wa kiwiko na kuona vidole
vyako vinaonekana kwa shida basi chakula cha asili kitakuwa kimekuwa cha
kutosha. Mbolea za asili ziwekwe kwenye bwawa kwa uwiano wa gramu 50 kwa kila
mita 1 ya mraba kila baada ya wiki moja. Hii ni sawa na wastani wa kilogramu 5
kwa kila kita za mraba 100 kwa wiki. Tazama jedwali hapa chini kwa maelezo
zaidi kwa kila aina ya mbolea.
Aina ya
Mbolea
|
Kg/wiki/m2
100
|
Kuku
|
2 had 3
|
Nguruwe
|
8 hadi 10
|
Ng'ombe
|
10 hadi 15
|
Mboji (Kuku 1:nguruwe2: ng'ombe 3)
|
10
|
ii) Bwawa likishatumika:
Kama bwawa lilishatumika kwa ufugaji
wa samaki, hakikisha unakaausha maji yote na kuliacha likauke kwa muda wa siku
14. Hii itasaidia kuua wadudu wote wa magonjwa na hatari kwa samaki pamoja na
kuharakisha uozeshaji wa mboji iliyokuweko kwa ufugaji ulipita kwenye udongo.
Hatua za urutubishaji zifanyike kama ilivyo katika bwawa jipya.
Wakati unarutubisha bwawa angalia
usiweke mbolea ndani ya bwawa ni virutubisho tu vinahitajika kuingia, angalia
kama samaki wanakuja juu na kuvuta hewa, weka mbolea asubuhi kuanzia saa nne
ili kuepuka upungufu wa oksijeni.
B) Uingizaji wa vifaranga
Mambo muhimu ya kuangalia wakati wa
kuchagua chanzo cha kupata vifaranga, uletaji kwenye bwawa na idadi ya kuweka
ndani ya bwawa na kama ifuatavyo:
i). Hakikisha chanzo unachukua
vifaranga ni cha uaminifu
ii) Chagua vifaranga vya samaki unaopenda
kuwafuga
iii) Weka kwenye bwawa idadi ya
vifaranga inayofaa kulingana na bwawa na aina ya samaki.
Kwa perege wa uzito wa gramu 20 hadi
40 weka vifaranga 1-2 kwa kila mita moja ya mraba na kama una mpango wa
kuchanganya na kambare, basi kwa kila vifaranga 1000 vya perege changanya
kambare 50 hadi 100 (asilimia 5-10 kwa idadi). Na kama unataka kufuga kambare
peke yake, weka vifaranga 2 hadi 5 kwa kila mita moja ya mraba. Ukitumia hiyo
idadi ya chini (vifaranga 2 kwa m2) tegemea kupata samaki wenye
gramu 500 kila baada ya miezi 6-9, lakini zaidi ya hapo utapata samaki wenye
uzito wa gramu 200 hadi 250 tu kutegemea na joto na matunzo unayowapa.
Kuweka samaki wengi mno (kushoto)
kunasababisha kuwe na samaki wengi lakini wadogo na kuweka samaki wachache
(katikati) kunafanya samaki wawe wakubwa lakini wachache wasiotosheleza uwezo
wa bwawa. Lakini kuweka kiasi sahihi (kulia) kunafanya upate samaki wakubwa na
bwawa kutumika vizuri.
iv)
Vifaranga wasipewe chakula kwa muda wa siku moja au mbili kabla ya
kuwasafirisha na hasa kama ni mbali.
vi) Safirisha samaki (vifaranga)
wakati ambapo hakuna joto na ni vizuri asubuhi au jioni sana
vii) Hakikisha vifaa
unavyosafirishia samaki haviwezi kuwasababishia michubuko au kuwachoma
vifaranga
viii) Muda wote wa kuwasafirisha
hakikisha samaki wapo kwenye maji
ix) Ukifika nao kwenye bwawa waweke
samaki kwenye bwawa maramoja lakini taratibu kwa kuwazoesha joto la maji
wanamoingia kwa kuzamisha pamoja na chombo.
x) Safisha vifaa vya kusafirishia
vizuri mara uwatoapo samaki
ULISHAJI WA SAMAKI CHAKULA CHA ZIADA
Chakula cha nyongeza kinasaidia
samaki wakue kwa haraka zaidi na kukuongezea kipato kwa kutoa samaki wenye afya
na kuvutia wateja. Mahitaji ya samaki huongezeka kadri wanavyo kua na kuzaliana
ndani ya bwawa na kufanya chakula cha asili kisiwatoshe au kipungue. Hivyo
watahitaji chakula cha ziada ambacho mara nyingi ni aina ya wanga nap rotini
kutoka kwenye pumba, mashudu ya pamba, dagaa, masalia ya chakula nyumbani
(ugali, wali n.k), na majani ya mimea mfano magimbi.Vyakula vya samaki vilivyotengenezwa
kiwandani kwa upande wa Tanzania na hata Afrika Mashariki havipatikani, hivyo
unaweza kutengeneza mwenyewe nyumbani. Hakikisha unasaga na kuchanganya vizuri
kabla hujawapa samaki. Mifano ya mchanganyiko yenyewe na kima inavyoonekana
hapa chini.
Mfano 1
|
Chakula
|
Asilimia (%)
|
Chakula cha
kilo 100
|
Mashudu (pamba au alizeti)
|
37
|
37
|
|
Pumba (Mahindi au mchele)
|
57
|
57
|
|
Dagaa
|
5
|
5
|
|
Vitamini na madini-changanya
|
1
|
1
|
|
Jumla
|
100
|
100
|
|
Mfano 2
|
|||
Dagaa
|
24
|
24
|
|
Pumba (mahindi au mchele
|
76
|
76
|
|
Jumla
|
100
|
100
|
Hakikisha unawalisha samaki chakula
cha kuwatosha tu na si zaidi ya hapo kwani kikiwa kingi kitaishia kuchafua maji
na itakuwa hasara tu. Swali hapa ni je utajuaje chakula cha kuwapa
kinachowatosha tu? Kwanza ni lazima ujue unasamaki wangapi ndani ya bwawa kisha
kadiria jumla ya uzito wa samaki wote ndani ya bwawa kwa kutafuta wastani wa
samaki wachache utakao wapima uzitowao.
Ni vizuri kupima uzito wa samaki
kila baada ya wiki mbili na wastani kwa samaki utumike kwa kulisha samaki,
asilimia 2 ya uzito wa samaki wote itakuwa chakula cha kuwapa samaki. Na
walishe si chini ya mara mbili kwa siku na muda mzuri wa kuwapa chakula ni kati
ya saa 4 asubuhi na saa 10 jioni kwani wakati huu viwango cha joto la maji
pamoja na oksijeni ni vya kutosha. Ukitumia mfano wa chakula cha pili hapo juu
utalisha kama inavyoonyesha katika jedwali hapa chini.
Muda tangu
uanze kufuga (miezi)
|
Makadirio ya
uzito wa samaki (gramu)
|
Kiasi cha
chakula kwa siku (g/samaki)
|
|
Pumba
|
Dagaa
|
||
1 hadi 2
|
5 hadi 20
|
1
|
1
|
2 hadi 3
|
20 hadi 50
|
1 hadi 3
|
1 hadi 2
|
3 hadi 5
|
50 hadi 100
|
3
|
2
|
5 hadi 8
|
100 hadi 200
|
4
|
3
|
Zaid ya 8
|
Zaidi ya 200
|
5
|
3 hadi 4
|
Upandewenye kina kifupi wa bwawa
ndio unaofaa kulishia samaki maana itasaidia kuona kama samaki wamekula chakula
chote au la. Samaki hukosa hamu ya kula endapo maji ndani ya bwawa ni ya baridi
sana au kama hewa ndani ya bwawa ni kidogo sana. Hvyo si kila chakula
kinapobaki humaanisha samaki wameshiba la hasha yaweza kuwa hali ya hewa
inasababisha wasile vizuri na kusababisha ukuaji hafifu.
MAREJEO
1. Katule A.M., Mnembuka B.V.,
Madala N., Lamtane H.,Mnubi R. 2010. Ufugaji mseto wa samaki. Kimechapishwa na
mradi wa pantil, SUA, Morogoro, Tanzania.
2. Ngugi C.C., Bowman J.R., Omolo
B.O. 2007. A New Guide to Fish Farming in Kenya, Aquaculture Collaborative
Research Support Program
3. Aquanews, 2007. Training Fish
Farmers in Tanzania, AquaFish Collaborative Research Support Program
Newsletter, Volume 22, Number 3
4. Bernard T. A CASE STUDY ON FISH
FARMING IN UGANDA
5. Rice A.M., Mmochi A.J., Zuberi L., Savoie R.
M. 2006. Aquaculture in Tanzania. World aquaculture, pp50-57.
Asante sana kwa maelezo mazuri
ReplyDelete