Wednesday, 1 March 2017

MWENDELEZO KILIMO BORA CHA MAHINDI

WADUDU WAHARIBIFU NA MAGONJWA YANAYOSUMBUA ZAO LA MAHINDI NA NJIA ZA KUDHIBITI
A) VIWAVI JESHI Ni wadudu aina ya funza ambao hutokana na Nondo.Hushambulia mahindi kwa kula majaniyake pamoja na shina. Wadudu hawa huangamizwa/kudhibitiwa kwa njia zifuatazo;-
  • Kuondoa vichaka karibu na shamba
  • Kunyunyizia sumu za asili kama vile Mwarobaini majuma mawili ya mwanzo.
  • Kunyunyizia sumu za viwandani endapo wadudu wameanza kuonekana km vile Karate 1ml/1l
B) FUNZA WA MABUA (MAIZE STALK BORER).
  • Funza wa mabua hutoboa shina la mahindi na kusababisha kudumaa kwa mahindi.
  • Matundu, ungaunga kama wa msumeno huonekana kwenye majani yaliyoathiriwa.
  • Mashambulizi huanza juma la pili hadi la tatu baada ya mahindi kuota.
NJIA ZA KUDHIBITI ZINAZOTUMIKA
  • Kuchanganya mahindi na mazao jamii ya mikunde km vile maharagwe
  • Kung’oa mahindi yaliyoshambuliwa
  • Sumu za asili mwarobaini
  • Sumu za viwandani km vile Karate
C)MAIZE STREAK DISEASE (VIRUS)
Dalili za ugonjwa huu huanza kuonekana kwa jani la mhindi kuwa na rangi nyeupe-njano.jinsi mhindi unavozidi kukua ndivyo dalili zake huonekana zaidi, gonjwa hili pia huashilia ukosefu wa madini chuma katika mmea
·         Tumia mbegu zinazostahimili gonjwa hili kama vileTMV-1, KILIMA ST, KATUMANI ST na STAHA
·         Panda mapema mahindi kwani gonjwa hili linashambulia sana wakati ikitokea umechelewa kupana
·         Tumia dawa za viwandani endapo tatizo hili litakua sugu
D). LEAF RUST
Kuna aina mbili za gonjwa hili la leaf rust.ambazo ni common leaf rust na polysora rust
Common leaf rust
Gonjwa hili hutokea pale mmea unapoanza kutoa ua la uchavushaji,,,hutambulika kwa kuonekana kama unga unga katika jani, na eneo lililoathiliwa na gonjwa hili huwa na rangi ya kahawia katika hatua za mwanzo na baadae hubadilika kuwa jeusi pale mmea unavokomaa na kusababisha mmea kuzorota au kufa kabisa.
Polysora leaf
Hasa hasa hupatikana katika maeneo yenye uwanda wa chini,eneo lenye unyevu unyevu hapa Tanzania.
·         Panda mapema ili kuzuia gonjwa hili
·         Badilisha badilisha mazao(msimu huu ukipanda mahindi katika eneo hilo msimu ujao panda maharagwe au zao lolote lenye jamii ya mikunde ili kuongeza rutuba)
UWEKAJI MBOLEA KATIKA MAHINDI
MATUMIZI YA MBOLEA
Mahindi hustawi zaidi yakiwekwa mbolea, iwapo mambo mengine yanayosaidia katika kukua pia yapo kwa kiwango kinachostahili. Mbolea inayotumiwa na wakulima wadogo mara yingi huwa haitoshi. Mahindi ya kiwango cha juu yaweza tu kufikia kiwango cha juu cha Uzalishaji iwapo yatapewa lishe na madini ya kutosha. Mahindi ya tani 2 kwa hekta na tani 5 kwa hekta hutumia karibu kilo 60 N, kilo 10 za P205 na kilo 70 K20 kutoka katika udongo. Mahindi hunyonya Nitrogen pole pole katika miezi ya kwanza baada ya kupanda, lakini huongezeka hadi kiwango cha juu kabisa wakati wa kutoa maua na kukuza tunda (gunzi). Mahindi huhitaji nitrogen kwa kiwango cha juu na ukosefu huwa ndio kizingiti. Kiwango cha juu cha nitrogen kinahitajika mara tatu; kwanza wakati wa kupanda, pili, wakati ambapo mmea umefikia sentimita 50 za urefu na tatu, wakati matunda ya mahindi yanaanza kutoa zile nyuzi nyuzi nyororo (silking).Udongo mwingi huwa na madini ya phosphorous (P205) na potassium (K20) lakini sio kiwango kinachotosheleza mahitaji haswa ya mbegu za mahindi zinapochipua. Nyunyuzia P205 karibu na mbegu ili ziote kwa haraka. K20 hutumika kwa kiwango kikubwa lakini hitaji la mimea hubainika baada ya upimaji wa hali ya udongo kujua kiasi cha mahitaji (soil test).Mbolea ambazo zina chumvi chumvi na zenye kuyeyuka haraka kwenye maji huleta madhara yafuatayo:
·         Huzuia viumbehai kukua hivyo kuharibu udongo.
·          Hulazimisha mimea kutumia hizi chumvi chumvi hata kama mimea haizihitaji.
·         Mimea inapotumia hizi chumvi chumvi kwa kulazimishwa ukuaji wake huvurugika na kusababisha upungufu wa afya na kinga hivyo kufanya mimea iweze kuathiriwa na magonjwa pamoja na wadudu.
Inashauriwa kutumia mbolea ambazo ni endelevu/hai na haziyeyuki haraka kwenye maji kwa mfano samadi, mboji na mabaki ya mimea ambazo ni nzuri kwa udongo, mimea, mazingira, afya na faida zake ni za muda mrefu. Kama ukitumia samadi au mboji, inashauriwa kuchanganya mbolea hizi katika udongo kabla ya kupanda mahindi ili kusaidia kurutubisha ardhi na kuupa mmea chakula na nguvu, baada ya mimea kuota inatakiwa kuendelea kuweka mbolea hizi mara kwa mara. Pia mbolea hai/endelevu husaidia kuhifadhi unyevu nyevu na kupunguza ukaukaji wa udongo. Madini ya nitrogen, phosphorous na potassium hupatikana kwenye mbolea hai kama vile samadi, mboji, mimea mibichi yenye uwezo wa kutengeneza nitrogen, mkojo wa mnyama na majivu. Inashauriwa kuhakikisha kuwa udongo wako unapitisha hewa ya kutosha ili kusaidia viumbehai waishio kwenye udongo wanaozalisha hivi virutubisho kuweza kukua.

MBOLEA ZA KUKUZIA
Ni mbolea zinazotumika baada ya mimea kuota kwa lengo la kuikuza mimea ili itoe mavuno bora. Mara nyingi mbolea hizi zinatoa kirutubisho cha naitrojeni. Mbolea maarufu za kukuzia katika soko la Tanzania ni kama:
Aina za mbolea
Kiwango cha kirutubisho cha naitrojeni 
Urea
46%
Calcium Ammonium Nitrate (CAN)
23%
Sulphate of Ammonia (SA)
21%

 DALILI ZA UPUNGUFU WA MBOLEA
Ukosefu wa K20 husababisha ncha za majani kuwa na rangi ya njano na kuunda gunzi (cob)lisilo na punje hadi juu. Ukosefu wa P205 hufanya matawi kuwa na rangi ya samawati na mbegu zisizo laini. Dalili za ukosefu wa nitrogen ni majani ya rangi ya manjano na mimea dhaifu mifupi. Phosphate haifyonzwi haraka na mahindi na pia udongo mwingi wa nchi za joto hukosa madini hayo ya phosphate. Inashauriwa unyunyuzie mbolea ya kiasili kama samadi kabla ya kulimaili uboreshe hali ya udongo na kuongezea madini. Katika ukulima wa kiasili, (organic farming, Nitrogen (N) hutiwa kwenye udongo kupitia kwa upandaji wa mimea ya jamii ya mikunde (legumes) ambayo hutoa nitrogen katika hewa, Hata hivyo mapendekezo ya kimbolea yaliyo katika misingi ya uchunguzi wa udongo hutoa nafasi nzuri ya kupata kiasi kizuri cha mbolea bila kuweka kiwango cha chini au juu. Omba msaada kutoka kwa mafisa ugani wa kilimo waliyo katika eneo lako. Katika maeneo yanayo tegemea mvua kukuza mahindi, panda mbegu wakati wa mvua ya kwanza. Hii itaruhusu mizizi kunyonya madini yaliyotengenzwa na bakteria katika udongo. Maji yaliyosimama huyeyusha na kuondoa madini ya nitrogen kutoka katika udongo na kusababisha ukosefu wa Nitrogen

MANUFAA YA MATUMIZI YA MBOLEA
i). Kuongeza mavuno
ii). Ubora wa mazao
iii). Kuhifadhi rutuba ya udongo
iv). Kuongeza kipato kutokana na mavuno mengi na bora

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA
Ni muhimu kutumia mbolea za viwandani katika kilimo cha mahindi ili kumuwezesha mkulima kupata mavuno mengi. Lakini ikumbukwe kwamba matumizi ya mbolea ni lazima yaambatane na matumizi ya mbinu nyingine bora za kuzalisha mahindi, kama vile:
>Kuandaa shamba
>Matumizi ya mbegu bora
>Kupalilia
>Kupiga madawa ya kuzuia na kuua wadudu na magonjwa
>Kuvuna kwa wakati unaostahili
>Kuhifadhi vizuri mahindi
Kwa maelezo zaidi, muone au wasiliana na:
1.      Bwana/bibi shamba wako.
2.      Muuza pembejeo aliye karibu nawe.
3.      Kitivo chochote cha Kilimo, vyuo vikuu vya Kilimo, na taasisi zingine vya utafiti wa kilimo.



KUKOMAA NA KUVUNA
Kukomaa kwa mahindi hutofautiana kutokana na aina ya mbegu iliyotumika. Lakini mahindi mengi huwa yamekomaa baada ya miezi mitano hadi saba. Majani ya muhindi yakianza kukauka ni ishara kuwa mahindi yamekomaa na inashauriwa kuyavuna mara moja na kuyahifadhi vizuri ili kuzuia hasara ambazo zitatokea kutokana na kuharibiwa na magonjwa au wadudu shambani kama yakicheleweshwa

UVUNAJI
Uvunaji hufanyika kwa kutumia mikono kwa mashamba madogo na mashine (combine harvester) hutumika kwa ajili ya mashamba makubwa, Zao la wastani la mahindi ulimwenguni mnamo mwaka 2000 lilikuwa kilogramu 4255 kwa kila hekta. Zao la wastani nchini Marekani ilikuwa kilo 8600 kila hekta, huku mataifa yaliyo chini ya jangwa la Sahara la Afrika yakivuna kilo 1316 kwa kila hekta ya shamba. Zao la wastani katika taifa la Tanzania kati ya mwaka 2001-2005 lilikuwa kati ya gunia 15-19 kwa hekta (sawa na kilo 1350-1750) Ukilima kwa kuzingatia
ukulima wa kisasa na kanuni zake kwa Tanzania utavuna kilo 5000 kwa hecta (ukanda wa pwani) na kilo 7500 kwa nyanda za juu kama Iringa, Mbeya, Ruvuma, Arusha n.k
Kupukusua mahindi kwa kutumia mashine ya mkono
3.    UHIFADHI WA MAHINDI
Mahindi huifadhiwa ghalani baada ya kuwekwa viatilifu vya kuzuia bungua wa mahindi Njia za kisasa za uhifadhi hutumiwa kama vile matumiz ya ACTELLIC SUPER DUST katika uwiano wa 1kg kwa gunia 5-10 za ujazo wa 100kg. Kiatilifu kingine ni actellic solution katika rate ya 5mls katika gunia moja la kg 100. Njia nyingine ya kienyeji katika kuhifadhi mahindi ni kuweka juu ya ghala ambalo chini yake kuna jiko la kupikia ambalo hutoa moshi unaotumika kufukuza na kuua wadudu. 
SOKO LA MAHINDI
Tanzania pamoja na nchi mbalimbali hapa duniani zinategemea zao la mahindi kama chakula, Hivyo katika hali kama hii tunaona kuwa ni jinsi gani zao hili la mahindi liliyvokua na umuhimu.katika hali ya kawaida,endapo mkulima atajikita katika ustawishaji wa zao hili ni lazima afaidike kwani mazao yake yatanunuliwa kwa urahisi na haraka endapo yatawekwa sokoni.
Katika maeneo tofauti tofauti hapa Tanzania, bei za mahindi zimekuwa tofauti tofauti lakini bei elekezi ya uuzaji wa mahindi kwa gunia ni TSH50,000 lakini bei hii imekua ikiteteleka kwa sababu ya vikwazo mbalimbali kama vile miundombinu mibovu ya barabara na magari au usafirishaji kwa ujumla ambavyo vinapelekea wakati mwingine bei kupanda na kushuka.


No comments:

Post a Comment