Thursday, 2 March 2017

KILIMO CHA VITUNGUU MAJI.

UTANGULIZI
Hapo awali kitungu kilikuwa ni zao lililokuwa linapatikana porini katika ukanda wa bahari ya Mediterania. Zao hili hulimwa katika nchi nyingi za magharibi, nchi za milima zilipo kaskazini mwa dunia, likwemo bara la Afrika. Vitunguu hustawi katika hali ya hewa ya jotoridi 13°C – 24°C, hali ya hewa inayofaa kwa kuotesha na kukuzia miche kwenye kitalu ni jotoridi la
20°C – 25°C. Kwa kawaida vitunguu huhitaji kiasi cha joto nyuzi 20°C-25°C ili kuweza kustawi na kukua vizuri. Joto zaidi ya hapo hufanya vitunguu kudumaa na kutoweza kutengeneza viazi (bulbs).Zao la kitunguu huhitaji unyevu muda wote wa ukuaji wake. Zao hili lina mizizi mifupi hivyo linahitaji kumwagiliwa maji mara kwa mara.. Nchini Tanzania, vitunguu maji hulimwa kwenye mikoa ya Iringa wilaya ya Kilolo mpakani mwa mkoa wa Morogoro na kwenye maeneo ya mto Ruaha,mkoani Arusha sehemu za Mang’ora na Babati, Kilimanjaro, na
Morogoro wilayani Kilosa sehemu za Lumuma na Malolo na baadhi ya sehemu za Mkoa wa Singida.

HALI YA HEWA.
Hali ya hewa ifaayo ni ile ya ubaridi wastani. Joto linalohitajika ni kati ya nyuzi joto 13 hadi 24°C ingawa kwa miche iliyoko kwenye kitalu joto zuri ni la nyuzi 20 hadi 25°C. Joto la juu hufanikisha utengenezaji wa kitunguu na ukaukaji.
AINA YA VITUNGUU MAJI
Kuna aina nyingi ya vitunguu maji. Aina hizi zinaweza kutofautishwa kulingana na:
(i) rangi ya ganda la nje la kitunguu kilichoishavunwa;
(ii) radha (utamu au ukali) wa kitunguu chenyewe;
(iii) mahitaji ya mwanga katika uzaaji: kuna aina yenye kuhitaji siku fupi (mwanga wa saa 10 hadi 12 kwa siku) na aina ihitajio siku ndefu (saa 13 hadi 14 za mwanga kwa siku) ili kuweza kuweka kitunguu.

Aina za vitunguu.
Aina
Siku za
kukomaa
Umbile la kitunguu
Rangi ya
ganda
Rangi ya
ndani
Red
Creole
150
Nusu bapa
Nyekundu
Nyekundu kahawia
Red
Bombay
160
Duara
Nyekundu angavu
Nyekundu kahawia
Texas
Grano
165
Duara
Njano (kaki)
Nyeupe

Uchaguzi wa mbegu za vitunguu vya kupanda kwa ajili ya biashara ni lazima uzingatie yafuatayo;-
mahitaji ya soko (vitunguu vyekundu hupendwa zaidi)
musimu wa kupanda
uwezo wa kuzaa mazao mengi
uwezo wa vitunguu kuhifadhiwa kwa muda mrefu.
Mbegu bora
·         Ubora wa mbegu ni muhimu sana, kwani ndiyo chanzo cha mazao bora.
·         Mbegu bora inatoamiche yenye afya na kuzaa mazao mengi na bora.
·          Mbegu za vitunguu inapoteza uoto wake upesibaada ya kuvunwa (mwaka1).
Mbegu nzuri zina sifa zifuatazo:-
·         Uotaji zaidi ya 80%
·         Mbegu safi zisiyo na mchanganyhiko
·         Zimefungwa vizuri kwenye vyombo visivyopitisha hewa na unjevu.

Hivyo mkulima anaponunua mbegu za vitunguu azingatie yafuatayo:-
·         Chanzo cha mbegu
·         Tarehe ya uzalishaji
·         Tarehe ya kuisha muda wake
·         Kifungashio cha mbegu.
·         Inashauriwa  mbegu zenye umri zaidi ya mwaka mmoja zisipandwe kwani uwezo wa kuota huwa mdogo sana.
Mbegu bora za vitunguu zinauzwa na makampuni binafsi kama: ALPHA Seed Co., Popvriend,
Rotian Seed, Kibo Seed, East African Seed Company nk. Wasambazaji wa mbegu ni pamoja namaduka ya TFA, na maduka ya bembejeo za kilimo katika maduka mbalimbali.

Jinsi ya kuandaa kitalu na kuzalisha miche.

Mbegu za vitunguu huoteshwa kwanza kwenye kitalu kilichoandaliwa vizuri takribani wiki mbili. Vitunguu maji huoteshwa zaidi kwa kutumia mbegu kwenye kitalu na kisha kupandikizwa shambani.Sehemu ya kitalu ni lazimaa iwe wazi, mbali na kivuli na kiwe karibu na chanzo cha maji.
Tengeneza tuta la ukubwa wa 1m x 2m . Urefu na idadi ya matuta hutegemea kiasi cha
mbegu. Kiasi cha mbegu kwa hekta moja ni kilo 6 au 2 kg kwa eka.
Weka samadi iliyooza vizuri kiasi cha debe moja au mchanganyiko wa mbolea ya TSP na
CAN (200gm) kwa uwiano wa 1:1 kwenye tuta changanya vizuri na udongo.
Sia mbegu kwenye mistari kwa nafasi ya 1 sm x 20 sm. Tawanya mbegu vizuri wakati
wa kusia ili miche isisongamane.Funika mbegu na weka matandazo ya nyasi kavu juu ya tuta na mwagilia maji. Udongounatakiwa kuwa na unyevu kiasi mpaka mbegu ziote.
Nyasi ziondolewe mara tu mbegu zikiota (siku7-10 kutegemea hali ya hewa).
Miche itunzwe vizuri na kitalu kiwe katika hali ya usafi.
Miche imwagiliwe maji mpaka ifikie umri wa kupandikiza shambani (wiki 5-6)
Matatizo ya miche kitaluni ni kama yafuatayo:-
1.Kuoza kwa mbegu, kunyauka kwa miche kabla na baada ya kuota. Hali hii inasababishwa naugonjwa wa ukungu.
-.Dawa za ukungu kama Dithane M45 au Ridomil MZ,nk,huweza kudhibiti ugonjwa huo kwa kuchanganya dawa na povu la sabuni ya mcheili dawa ishike kwenye majani.
Piauangalifu uwepo wakati wa kumwagilia maji. Mwagilia maji wakati wa asubuhi au jioni.


NB;
Epuka kumwagilia maji wakati wa jua kali kwani unjevunjevu hewani unaongeza na kusababishavimelea vya magonjwa.
Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa wekunduambao wanashambulia majani katika kitalu ,
Sota,ambaohukata miche na kusababisha vitunguu kukauka.
-Dawa za viwandani kama Thiodan , Selecron au Dusrban zinazuia na kudhibitihawa wadudu.

KUPANDIKIZA VITUNGUU SHAMBANI

Baada ya wiki 5 au 6, kutegemeana na hali ya hewa miche itakuwa tayari kupandikizwa
shambani. Miche iimarishwe kwa kusitisha maji, wiki moja kabla ya kupandikiza.
Shamba liwe sehemu isiyokuwa na mwinuko, sehemu ya wazi ambayo haijalimwa
vitunguu kwa muda wa miaka 2 -3. Shamba liwe karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya
umwagiliaji. Matuta 1m x 3m au majaruba ya 2mx 3m.yanafaa kwa kupanda miche. Matuta au
majaruba yanarahisisha umwagiliaji, palizi na unyunyiziaji wa dawa.
Miche hupandikizwa inapokuwa na urefu wa sentimita 10- 15 na unene 1/2 au 3/4 ya penseli kwenye shina. Miche hii huwa imetimiza umri kati ya wiki 7 hadi 9 kulingana na matunzo. Miche inapandikizwa kwenye nafasi ya upana wa sentimita 20 hadi 30 na nafasi ndani ya mstari ni sentimita 10 hadi 15.

Matumizi ya mbolea

Vitunguu maji vinamahitaji makubwa ya rutuba ya udongo. Hukua vizuri vinapopata samadi ya kutosha kiasi cha tani 25 hadi 40 kwa hekta. Mbolea isambazwe shambani baada ya kupandikiza, lakini ni vizuri zaidi kama ikichanganywa kwenye udongo kabla ya kupandikiza. Kwa kuzingatia mazao ya tani 18 kwa hekta, vitunguu huchukua virutubisho kutoka kwenye udongo, kiasi cha wastani wa kilo 66 za nitrojeni, 11 za fosiforasi na 70 za potasiumu.Hivyo kiasi cha mbolea kinachopendekezwa ni kilo 450 hadi 565 za mbolea ya NPK (10-10-20) kwa hekta. Mbolea huwekwa siku 7 hadi 10 kabla ya kupandikiza. Kisha, inapendekezwa kuweka kiasi cha kilo 13 hadi 18 za Nitrojeni baada ya wiki tatu hadi nne, ili kuongeza ukuaji wa mimea. Upungufu wa kirutubisho cha Nitrojeni unaharakisha ukomaaji na unapunguza ukubwa wa kitunguu. Kirutubisho hiki kikizidi kupita kiasi huongeza ukubwa wa kitunguu na unene wa shingo ya kitunguu, tabia ambayo hupunguza ubora.
UMWAGILIAJI:
Umwagiliaji mzuri unahitajika ili kupata vitunguu bora. Umwagiliaji wa maji yanayokwenda chini kiasi cha sentimeta moja au zaidi kwa wiki ni mzuri kwa kupata vitunguu vikubwa. Epuka umwagiliaji kupita kiasi au pungufu kwani hali hii huweza kusababisha mipasuko wa vitunguu.


UDHIBITI WA MAGUGU
Ukuaji na mavuno yanaathirika sana endapo magugu hayatadhibitiwa mapema. Magugu yanadhibitiwa kwa kutumia madawa ama jembe dogo la mkono. Wakati mwingine ni mchanganyiko wa madawa, jembe la mkono na kung’olea kwa mkono.
UDHIBITI WA MAGONJWA

1.      Ukungu wa unga (powdery mildew) na wa chini (Downy
mildew)
Magonjwa haya hushambulia majani ya mimea shambani na hata miche michanga. Kwenye majani kunaonekana vidoa vyeupe hasa kwenye majani makuu ya mimea michanga. Ukungu mweupe unatokea na kuongezeka kwa haraka kwenye sehemuza baridi au nyakati za baridi. Viini huishi kwenye mabaki ya mimea ya vitunguu na huweza kupeperushwa mbali na upepo. Kwenye mimea michanga ugonjwa unaweza kudhibitiwa na madawa kama mancozeb,Dithane-M45, Ridomil, Topsin M70 na Cupric Hydroxide (Champion).

 2.  Ugonjwa wa doa la pinki (Purple blotch)
Huu nao ni ugonjwa uletwao na Ukungu na hushambulia majani, shingo na vitunguu vilivyokomaa. Huanza kama doa dogo linalozama ndani ya jani na kisha linaongezeka ukubwa na kufanya baka la rangi ya Zambarau ambalo huonekana katikati ya jani ambalo baadaye huwa jeusi. Shina lililoshambuliwa hulegea na kuanguka katika wiki ya tatu au ya nne baada ya dalili za ugonjwa kuonekana. Vitunguu vilivyokomaa huoza kuanzia shingoni na hugeuka rangi kuwa ya njano iliyochanganyika na nyekundu.

jinsi ya kuzuia ugonjwa.

Zuia ugonjwa huu kwa kufanya yafuatayo:-
  •  Kupanda aina ya vitunguu visivyoshambuliwazaidi na ugonjwa huu mfano Red Creole.
  •  Kubadilisha mazao
  • Vuna vitunguu kwa wakati sahihi
  • Matumizi ya mbolea zenye kalisiamu, fosifeti napotashiamu hupunguza kuenea kwa ugonjwa huu.
  •  Kwa upande mwingine,matumizi ya mbolea ya nitrojeni kwa wingi au kwa kiasi pungufu huongeza mlipuko wa magonjwa.
  • Viatilifu kama vile Mancozeb Dithane-M45, Ridomil, Topsin M70 na Cupric Hydroxide (Champion).

   3.Kuoza kwa shingo (Neckrot)
Husababishwa na ukungu na hupendelea vile vile hali ya unyevunyevu. Hushambulia zaidi vitunguu vilivyohifadhiwa. Ugonjwa huu husababisha vitunguu kuwa laini, hubonyea na huonekana kama vilivyopikwa. Huanzia kwenye shingo na baadaye huenea kwenye kitunguu chote na kufunikwa na ukungu wa kijivu.
Namna ya kuzuia:-
  • Vuna vitunguu kwa wakati sahihi 
  • Kubadilisha mazao 
  •   Tumia njia sahihi wakati wa kuvuna, epuka kuchubua au kukikwaruza wakati wa kuvuna
  •   Kausha vitunguu vizuri baada ya kuvuna

Hali hii inaweza kutokea shambani au wakati wa hifadhi ghalani. Ugonjwa huu ni hatari zaidi kwenye sehemu za joto na zenye kutuamisha maji. Ni vyema kuhakikisha kwamba shambani hakuna hali ya kutuamisha maji na pia kwenye ghala kunakuwa na hali nzuri ya mzuunguko wa hewa.
4.Kinyausi (Damping – off)
 Ugonjwa huu unasababishwa na fangasi na kuenezwa na udongo, mbegu na masalia ya mazao.
Ugonjwa huu unasababisha mbegu kuoza kabla ya kuota na kunyauka kwa miche baada ya kuota.
Ugonjwa unajitokeza hasa kitaluni ikiwa hali ya hewa ina unyevunyevu na udongo una maji
maji.
Njia za kudhibiti ni kama zifuatazo:-
·         mbegu ziwe safi na ziwekwe dawa ya thiram
·         kutumia mzunguko wa mazao
·         kusia mbegu kwa nafasi za kutosha
·         kuepukana na kubananisha miche kitaluni
·         kuepuka kumwagilia maji wakati wa jua kali au wakati kuna ukungu

5.Virusi njano vya vitunguu (Onion yellow Dwarf virus)
Ugonjwa huu unasababishwa na virusi na kuenezwa na wadudu aina ya vidukari (wadudu
mafuta).
Dalili za ugonjwa ni:-
·         mistari ya rangi ya manjano kwenye majani.
·         kujikunja kwa majani
·         majani kugeuka rangi ya manjano na kuanguka
·         mmea mzima kudumaa, kujikunja na kufa.
Njia za kudhibiti ugonjwa huu ni:-
·         kutumia mbegu safi
·         kuweka shamba katika hali ya usafi


UDHIBITI WA WADUDU
Utitiri wa vitunguu (Onion thrips), Funza wa vitunguu (Onion maggots) na Minyoo ya vitunguu (Onion wireworms) ni miongoni mwa wadudu wasumbufu kwenye zao la kitunguu.
1. Utitiri wa vtunguu (Onion thrips)

Hawa ni wadudu wadogodogo sana ambao hula kwa kukwaruza juu ya jani na kunyonya majimaji ya kwenye mmea. Hali husababisha kutoka kwa mikwaruzo myeupe kwenye majani ya vitunguu. Mashambulizi yakizidi majani huanguka na kunyauka. Ukubwa wa
vitunguu hupungua. Hili ni tatizo kubwa zaidi hasa wakati wa ukame kuliko wakati wa unyevu hivyo athali ni kubwa wakati wa kiangazi.
2.      Bungua weupe (White grub)
Huyu ni aina ya funza mkubwa. Hutaga mayai yake kwenye uozo wa majani na samadi na hivyo mashamba ya vitunguu yaliyoko karibu au kwenye maeneo ya jinsi hiyo huwa kwenye hatari zaidi. Hushambulia mizizi na kusababisha kukauka kwa mimea. Kutifulia shamba na kuwaweka wazi wadudu hawa kunapunguza idadi yao.


3.Vipekecha majani (leaf miners).
 Hawa ni aina ya nzi wadogo, ambao viwavi wake wanashambulia majani, kwa kupekecha na
kutengeneza mitandao ya mitaro kwenye majani. Viwavi wanashambulia majani na
kusababisha majani kukauka. Upungufu mkubwa wa mazao hutokea.
Njia ya kudhibiti:
·         kupulizia dawa ya wadudu kama karate, Selecron na Dursban.
·         kuteketeza masalia ya mazao.
·         kutumia mzunguko wa mazao.

KUVUNA NA KUHIFADHI VITUNGUU

Kabla ya kuvuna vitunguu kagua shamba ili kuhakikisha kuwa vitunguu vimekomaa.
Dalili ya vitunguu kukomaa ni:-
·         majani kunyauka na kuanza kukauka
·         asilimia 75 -100% kuangusha shingo na majani kukauka.

Kuvuna

Vitunguu vinavunwa kwa mikono. Mimea inang’olewa au kuchimbuliwa kwa kutumia rato
(jembe uma). Baada ya kuvuna vitunguu vinaweza kuachwa shambani vikiwa vimefunikwa na
majani kukinga jua kali kwa muda wa siku mbili au tatu kutegemeana na hali ya hewa. Lengo ni
kuimarisha ngozi ya vitunguu na kufanya michubuko na majeraha madogo madogo yanayotokea
wakati wa kuvuna kuwa magumu na kutengeneza mokovu ambayo yanazuia vimelea vya
magonjwa kuingia ndani. Pia kupunguza unyevu kwenye majani na mashina na kuruhusu
sehemu ya chini ya shingo kufunga. Ikiwa usalama ni mdogo, vitunguu vinachambuliwa na
kukatwa majani na mizizi na kuanikwa sehemu nyingine.
Kuchambua

Tenga vitunguu vilivyooza, kuchubuka na kupasuka. Vitunguu vizuri vikaushwe peke
yake.
Iwapo vitunguu vitahifadhiwa kwa kuning’iniza kwenye chaga, basi shingo zisikatwe, bali
zisukwe na kufungwa pamoja, na kuning’inizwa.

Kukausha

Hatua hii ni muhimu ili kupunguza unyevu, kufanya vitunguu viwe vigumu na kuwa katika hali
ya kulala bwete.Vitunguu vinaweza kukaushwa kwa kuninginiza kwenye chaga zilizopangwa
mfano wa dari ndani ya banda au kutandaza kwenye kichanja chenye kuruhusu mzunguko wa
hewa pande zote, chini ya kivuli sehemu kavu. Epuka kukausha vitunguu chini ya aridhi
na hasa sehemu zenye jua kali. Jua linababusha vitunguu na kusababisha uharibifu. Ukaushaji
huchukua muda wa siku 7 au zaidi kutegemeana na hali ya hewa.

Kupanga madaraja

Vitunguu vinachambuliwa tena baada ya kukausha ili kuondoa vitunguu vyote vyenye ugonjwa
au dalili za ugonjwa, vilivyoota na kutoa mizizi na vyenye shingo nene. Vitunguu vinapangwa
kwenye madaraja mbalimbali kufuata ukubwa, umbo au rangi. Hii inawezesha kupata soko zuri
na kuepuka upotevu mkubwa wakati wa kuhifadhi.

Kufungasha na kuweka vitambulisho.

Vifungashio vinavyopatikana ni mifuko ya nyavu vyenye uwezo wa ujazo wa kilo 20 au
magunia ya katani. Mifuko ya nyavu ina ujazo mdogo na pia inarahisisha ubebaji. Magunia ya
katani yanatumika lakini yanaficha vitunguu visionekane pia vinachukua mzigo mzito na kuleta
usumbufu wakati wa kupakia na kupakua.
Vitambulisho vinawekwa kwenye vifungashio ili kusaidia wasafirishaji kujua mzigo ulikotoka
na pia kutangaza bidhaa inayohusika kwenye masoko ya nje na ndani.

Kwa soko la nje ya nchi, vitambulisho vinatakiwa kuwa na habari zifuatazo:

Jina la bidhaa mfano. Vitunguu Mango’la Red
Uzito kamili mfano. 20 kg
Jina na anwani ya mkulima au kikundi, jina na anwani ya msafirishaji
Jina la kijiji wilaya, Mkoa na nchi mfano. Igurusi, Mbarali, Mbeya, Tanzania
Grade 1

Kwa soko la ndani ya nchi,vitambulisho vinakuwakuwa  na habari zifuatazo:
·         Jina la bidhaa.mfano.vitunguu Mango,la Red
·         Uzito kamili mfano. 20 kg
·         Jina la mkulima au kikundi na anwani mfano,HEBRON VENANCE au JITEGEMEE, Box 200, Mbarali-Mbeya
·         Jina na anwani ya msambazaji mfano:Mr. NEBART CHALAJI Box 172, Mbarali.
Usafirishaji wa vitunguu.
Uangalifu wakati wa kupakia, kusafirisha na kupakua ni muhimu ili kuepukana na uharibifu na
upotevu wa vitunguu. Mara nyingi vitunguu vinaharibika kutokana na ujazo kupita kiasi kwenye
vifungashio na vyombo vya usafiri, pia kutokana na upakiaji na mpangilio mbaya, ambao
unasababisha ugandamizaji na kubonyea kwa vitunguu.
Wakati wa usafirishaji yafuatayoyazingatiwe:-
·         kutumia vyombo vya usafiri vinavyofaa hasa magari yenye nafasi ya kutosha na yenyekupitisha hewa.
·         kupanga mifuko katika tabaka zenye safu zisizidi tatu.
·         mifuko isitupwe wakati wa kupakia na kupakua.
·         vitunguu visichanganywe na mazao mengine.
KUHIFADHI
Vitunguu vinahifadhiwa kwenye maghala bora kama kribu au mabanda ambayo yanaruhusu
hewa na paa kuezekwa kwa nyasi ili kupunguza joto.
Utengenezaji wa kribu.
Kribu inajengwa kwa fito au mianzi na kuinuliwa juu mita moja toka usawa wa aridhi. Upana
wa kribu uwe kati ya sm 60 na 150 ili kuruhusu upepo kupita kwa urahisi. Upepo unaondoa
unyevu na joto kwenye vitunguu. Kribu igawanywe sehemu mbili zenye kina cha sm 60 kila
moja na kutenganishwa na uwazi was m 30, ili kuruhusu mzunguko wa hewa.
kutengeneza kribu yaafutayo yazingatiwe:-
·         Kribu ijengwe kwenye sehemu yenye upepo
·         Kribu iezekwe kwa nyasi ili kudhibiti joto na jua
·         Miguu ya kribi iwekwe vizuizi vya panya.
·         Weka vitunguu tabaka mbili na kina cha vitunguu kisizidi sm 60
·         Hifadhi kwa kuning’iniza vitunguu kwenye banda
Hili ni banda lenye uwazi mkubwa, lenye upana usiozidi mita tano, na urefu toka chini hadi
juu usizidi mita 2½. Banda linajengwa kwa miti, fito, mbao au mianzi na vitunguu
vinahifadhiwa kwa kuning’iniza kwenye fremu za fito ndani ya banda. Safu za vitunguu
hupangwa kufuata urefu wa banda na kimo cha banda. Urefu wa banda huelekezw a kwenye
mkondo wa upepo ili kuruhusu upepo kuingia na kutoka. Banda liezekwe kwa nyasi ili
kudhibiti joto na jua. Kribu au banda vinahifadhi vitunguu vizuri kwa muda wa miezi sita
bila kuharibika.
Upotevu wa vitunguu ghalani.
Vitunguu vingi hupotea wakati wa kuhifadhi kwa sababu ya:-
·         Kuoza
·         Kuota (toa majani na mizizi)
·         Kupoteza uzito
a)      Kuoza
Kuoza kwa vitunguu vikiwa ghalani kunasababishwa na vimeliea vya fangasi au bacteia. Joto
pamoja na unyevunyevu ndani ya ghala, kunasababisha kuzaliana na kuongezeka kwa vimelea
vya magonjwa
Kudhibiti:
-Weka ghala katika hali ya usafi, kausha vizuri na chambua vitunguu kabla ya
kuhifadhi.
b)     Muozo Kitako (Bottom rot or basal rot)
Vimelea vya aina ya fangas vinavyoishi kwenye udongo, vinashambulia sehemu ya chini ya
vitunguu. Vimelea hupenya kwenye sehemu zenye michubuko, inayotokea wakati wa palizi,
kuvuna au kusafirishwa.
Njia zifuatazohutumika kudhibiti:-
·         mzunguko wa mazao ghalani.
·         uchambuaji mzuri kabla ya kuhifadhi
·         kuepuka michubuko wakati wa palizi na kuvuna.
·         Kuwa na kucha fupi ili kuzuia michubuko kwenye vitunguu.
c)      Ukungu mweusi (Black mould).
Ugonjwa huu unaletwa na vimelea vya fangasi, vinavyoishi kwenye udongo. Vimelea
vinazaliana katikati ya maganda na ukungu mweusi kama poda unaonekana. Baadaye maganda
yanasinyaa na kuvunjika.
Kudhibiti ugonjwa huu;-
·         kutumia mzunguko wa mazao ghalani.
·         kukagua ghala mara kwa mara na kuondoa vitunguu vilivyooza
·         kuweka ghala katika hali ya usafi.
·         Kuondoa masalia ya vitunguu na kuchoma moto.
d)     Kuoza shingo (Neck rot)
Vimelea vya fangasi vinashambulia vitunguu vikiwa shambani kabla ya kuvuna. Ugonjwa
hauonekani mpaka vitunguu vikomae, vivunwe, vikaushwe na kuhifadhiwa ghalani, ndipo
ugonjwa hujitokeza. Ugonjwa unasababisha kuoza kwa vitunguu. Maganda ya vitunguu
yanalainika kuanzia shingoni na nyama ya kitunguu huwa na sura ya maji maji.
Vitunguuvilivyooza hunyauka na kusinyaa.
Kudhibiti;
·         kukausha vitunguu vizuri kabla ya kuhifadhi
·         kuchoma na kuharibu masalia ya vitunguu shambani na ghalani.
e)      Muozo laini (Bacterial soft rot)
Ugonjwa unasababishwa na vimelea vya bacteria. Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni kulainika
kwa vitunguu na kutoa harufu mbaya. Ukiminya kitunguu, maji yenye harufu mbaya hutoka
kwenye shingo. Muozo laini unatokea wakati hali ya hewa ikiwa na unyevunyevu na joto. Pia
vitunguu vyenye shingo nene ambavyo havijakauka vizuri ni sehemu nzuri sana ya vimelea
kuzaliana.
Kudhibiti :
Ukaushaji wa haraka na wa uhakika baada ya kuvuna unapunguza sana ugonjwa huu

Kuota na kupoteza uzito wa vitunguu
Vitunguu vinakuwa katika hali ya kulala bwete bila kuota kwa zaidi ya miezi sita ikiwa hali ya
hewa ghalani ni nzuri. Unyevunyevu mwingi ghalani ni adui mkubwa wa vitunguu
vilivyohifadhiwa kwani inasababisha kuota kwa majani na mizizi. Pia hewa ikiwa kavu sana
vitunguu hupoteza maji upesi na kusinyaa. Kuongezaka kwa joto na unyevunyevu ndani ya ghala
kutokana na mzunguko mbaya wa hewa, uchafu ghalani, ukaushaji na uchambuaji mbaya
vinasababisha uharibifu mkubwa wa vitunguu ghalani
Kudhibiti ;
·         Ghala liwe safi pia liwe na uwezo wa kupitisha hewa kavu na ubaridi wa kutosha.
·         Ghala lijengwe sehemu yenye upepo na kuruhusu mzunguko mzuri wa hewa.
·         Vifungashio vya vitunguu vipangwe vizuri ili kuruhusu hewa kupita juu na chini.
·         Vitunguu ndani ya kribu/ghala vijazwe kina cha sentimeta 30-50.
·         Vitunguu vichambuliwe vizuri kabla ya kuhifadhi.
·         Vitunguu ghalani vikaguliwe mara kwa mara ili kuondoa vitunguu vilivyoharibika

UUZAJI WA VITUNGUU

Watu wa aina mabalimabali wanahusika na ununuzi na uuzaji wa vitunguu wakiwa ni pamoja na:
wakulima, wachuuzi, wafanya biashara ndogondogo, wauzaji wa jumla, wauzaji wa rejareja, wasafirishajina madalali.
Ili koboresha uuzaji na kipato cha mkulima ni muhimu kuzingatia yafuatayo:
·         Kuboresha ujazo kwa kufuata vipimo vinavyokubalika (kufuta lumbesa).
·         Kupeana habari za masoko na bei kwa kutumia mitandao ya simu, kijamii na vyombo ya habari kama redio na magazeti.
·         Kuboresha usafirishaji kwa kutumia vikundi.
·         Kuwepo na mtiririko wa kuuza vitungu mwaka mzima, kwa kuboresha hifadhi ikiwa
·         Ni pamoja na maghala.
·         Kutathimini na kuzingatia ubora wa vitunguu.
·         Kutathimini na kuboresha ufungashaji na usafirishaji.


No comments:

Post a Comment