Monday, 13 March 2017

UFUGAJI WA NG'OMBE KISASA.

3

ORODHA YA MAJEDWALI.
Jedwali na. 4. Kiasi cha maziwa na chakula maalumu kwa ndama……………………………………………………………………….29
Jedwali na.5.  Umri na uzito unaoshauriwa kupandisha mtamba…………………………………………………........................32

SHUKRANI

Shukrani za pekee zinatolewa kwa walioshiriki kikamilifu katika urahisishaji wa uandaaji wa kitabu hiki kijitabu hiki hasa FARM Africa.
Shirika  la Isangati Agricultural Development Organiztion (IADO) pia linatoa shukrani za pekee kwa  kwa wadau wengine ambao utafiti wao kwa namna moja au nyingine umefanikisha kuandaliwa Kwa kitabu hiki.

UFUGAJI WA NG’OMBE.

A.UFUGAJI BORA WA NG’OMBE WA ASILI

1.0 .UTANGULIZI:

Ng’ombe ni mnyama jamii ya nyati ambaye hufugwa na mwanadamu. Nchini Tanzania ng’ombe ni mnyama mkubwa kuliko wanyama wengine wote wanaofugwa vijijini. Ng’ombe huwapatia wanadamu nyama, maziwa, ngozi na mbolea. Ng’ombe hufugwa katika  mikoa yote ya Tanzania.
Ufugaji holela wa ng’ombe ni ule usiozingatia kanuni na misingi ya ufugaji na una madhara makubwa. Madhara hayo ni pamoja na:
Ø   Kupata mapato duni
Ø  Uharibifu wa mazingira
Ø  Ugonvi na migogoro katika jamii.
Ø  Kutumia muda mwingi katika kuchunga badala ya shughuli nyingine
Ø  Ni rahisi ng’ombe kushambuliwa na kueneza magonjwa
Ø  Watoto hukosa elimu kwa kuwa hujihusisha na kuchunga ng’ombe
Ø  Malisho duni kutokana na kufunga ng’ombe kuliko uwezo wa nyanda husika
Ø  Ufugaji huu hauzingatii ubora bali wingi wa mifugo.

2.0. AINA ZA NG’OMBE WALIOPO NCHINI TANZANIA.

2.1.Ng’ombe wa asili

i. Zebu
ii. Ankole
iii. Boran

2.2. Ng’ombe wa Kigeni/Kisasa

i. Friesian
ii. Ayrshire
iii. Guensey
iv. Jersey
v. Brown Swiss
vi. Sahiwal

2.3.Ng’ombe Chotara

Ng’ombe chotara ni wale waliopatikana kutokana na kuchanganya damu za aina mbili au zaidi za ng’ombe wa kigeni na wa asili. Ng’ombe chotara wana sifa bora mchanganyiko za ng’ombe wa kigeni na asili. Mpwapwa; wamezalishwa kutokana na ng’ombe aina ya Boran, zebu, sahiwal na ng’ombe kutoka Ulaya.

3.0. SIFA ZA NG’OMBE WA ASILI.

i. Wana uwezo wa kustahimili magonjwa
ii. Hustahimili muda mrefu bila malisho yakutosha
iii. Wanaweza kutembea mwendo mrefu kutafuta maji na malisho
iv. Nyama na maziwa yao yana ladha nzuri
v. Maziwa yao yana mafuta mengi kuliko ya ng’ombe wa kisasa

3.1.Mapungufu ya ng’ombe wa asili

i. Wana umbile dogo
ii. Huchukua muda mrefu kuzaa (Ndama moja kila baada ya miaka mwili)
iii. Hutoa maziwa kidogo

4.0. KOO ZA NG’OMBE WA ASILI NA SIFA ZAO.

4.1.Zebu

i. Wana nundu
ii. Wana pembe fupi
iii. Wana umbo dogo
iv. Wana rangi nyingi tofauti tofauti katika sehemu mbalimabali
v. Wanapatikana katika mikoa yote ya Tanzania

4.2. Ankole

i. Ng’ombe jike hawana nundu ila madume wana nundu ndogo
ii. Wana pembe kubwa na ndefu
iii. Hushambuliwa na magonjwa zaidi kuliko Zebu
iv. Hutoa maziwa kidogo hivyo sio wazuri kuwafuga kwa ajili ya maziwa
v. Wanapatikana katika mikoa ya kanda ya ziwa Victoria

4.3. Boran

i. Wana umbile kubwa
ii. Wana nundu kubwa
iii. Wana pembe fupi na wengine hawana pembe
iv. Ni ng’ombe wa maziwa na nyama
v. Wana kua haraka kufikia uzito wa kuchinjwa
vi. Nyama yake huweka mafuta kiasi ni laini na yenye ladha
vii. Wana uwezo wa kuzaa ndama kila mwaka
viii. Huzaa ndama wenye uzito mkubwa
ix. Wanahitaji malisho mengi
Boran wanapatikana Kenya na Tanzania katika Ranchi za Taifa mfano Ranchi ya Manyara
na kwa baadhi ya wafugaji binafsi.

5.0. MIFUMO YA UFUGAJI WA NG’OMBE WA ASILI.

Kuna mifumo mbalimbali ya ufugaji katika uzalishaji wa ng’ombe wa asili.Mifumo hiyo ni:
i. Ufugaji huria
ii. Ufugaji huria uliochanganyika na kilimo
iii. Ufugaji kwenye ranchi
iv. Ufugaji wa kulisha vyakula vya nafaka kwa wingi

5.1.0.Ufugaji huria

Ufugaji huria ni mfumo wa ufugaji ambapo wafugaji huhamahama ili kutafuta malisho na
maji. Wafugaji hawa hutegemea mifugo kwa ajili ya mahitaji yao yote.

5.1.1 Faida za ufugaji huria

i. Ni njia ya kujihami na ukosefu wa maji na malisho hasa wakati wa ukame/kiangazi
ii. Gharama za kuendesha mfumo huu ni ndogo

5.1.2 Hasara za mfumo wa ufugaji huria

i. Mifugohupoteza nguvu nyingi kwa kutembea masafa marefu, na hivyo kuchukua
muda mrefu kukua na kufikia uzito wa kuchinjwa
ii. Ni vigumu kupatiwa huduma za kijamii kutokana na wafugaji kuhamahama.
iii. Mfumo huu husababisha uharibifu wa mazingira endapo mifugo itakuwa mingi.
iv. Kupungua kwa aina mbalimbali za nyasi na mimea katika nyanda za malisho.
v. Mfumo huu umekuwa chanzo kikubwa cha migogoro kati ya jamii za wafugaji na
wakulima.
vi. Ni rahisi kwa ng’ombe kuibiwa au kupotea.
vii. Ni rahisi mifugo kushambuliwa na wanyama wakali.

5.2.0. Mfumo huria uliochanganyia na kilimo

Huu mfumo wa kukuza ng’ombe wa nyama hapa Tanzania ambapo wafugaji pia ni
wakulima wa mazao hasa ya chakula. Ng’ombe huchungwa kwenye maeneo maalumu
yaliyotengwa mbali na mashamba ya mazao. Aidha baada ya kuvuna ng’ombe huchungwa
kwenye mashamba.

5.2.1. Faida za mfumo huria uliochanganyia na kilimo

i. Mfugaji huweza kuuza mifugo na kujipatia fedh za chakula iwapo mavuno ya
mazao yatakuwa pungufu.
ii. Samadi huweza kuboresha mbuga za malisho na mashamba.
iii. Mifugo pia huweza kufaidika na masalia ya mazao shambani baada ya mavuno.

5.2.2. Hasara za mfumo huria uliochanganyia na kilimo

i. Ni chanzo cha uharibifu wa mazingira
ii. Ni chanzo cha kuenea kwa magonjwa
iii. Ni chanzo cha migogoro kati ya wakulima na wafugaji

6.0. UBORESHAJI WA NG’OMBE WA ASILI.

Ng’ombe bora wa nyama na maziwa wanaweza kupatikana kutokana na kuchagua
ng’ombe wenye sifa nzuri kutoka katika kundi alilonalo mfugaji na kuwaruhusu wazaliane
ili kuendeleza kizazi.Uboreshaji huu wa ng’ombe wa asili unaweza kufanyika kwa
kupandisha majike ya asili.Mfano Zebu na madume ya asili kama Borani au madume ya
kisasa.

6.1.0. Uchaguzi wa ng’ombe bora

Mfugaji anashauriwa achague na aruhusu ng’ombe wenye sifa zifuatazo kuzaliana ili
hatimaye awe na kundi la wanyama walio bora.
i. Madume yenye maumbile makubwa yenye uwezo wa kupanda majike
ii. Majike yanayozaa ndama mwenye uzito mkubwa kila mwaka.
iii. Majike yenye kutoa maziwa mengi
iv. Majike yasiyopata matatizo wakati wa kuzaa.

6.1.1. Uchaguzi wa majike bora

i. Atokane na koo zenye uwezo wa kutoa maziwa ya kutosha kulisha ndama ili akue
haraka
ii. Awe na uwezo mkubwa wa kumlea ndama
iii. Astahimili magonjwa na kumudu hali ya mazingira anakofugwa
iv. Awe na uwezo wa kuzaa kila mwaka

6.1.2. Uchaguzi wa dume bora

i. Anayekuwa haraka
ii. Awe na uwezo wa kustahimili magonjwa na hali ya mazingira ya eneo la kufuga
iii. Awe na umbo halisi la dume bora
iv. Shingo kubwa
v. Kifua kipana
vi. Awe na miguu imara isiyokuwa na matatizo.
vii. Awe na uwezo wa kutambua majike yaliyo kwenye joto,kuyapanda kwa wakati
muafaka na kuweka mimba
viii. Awe na utulivu lakini siyo mwenye aibu na mgomvi
ix. Awe na mapumbu yanayolingana
x. Asiwe mgonjwa kama vile magonjwa ya zinaa ili kuepuka maambukizi kwa majike.

Angalizo:
Chagua dume asiye na mahusiano ya karibu na majike ili kupunguza kutokea kwa vilema
na magonjwa ya kurithi.

7.0. UZALISHAJI WA NG’OMBE WA ASILI.

Ng’ombe chotara ni wale waliopatikana kutokana na kuzalisha aina mbili au zaidi za
ng’ombe wa kigeni na wa asili. Ng’ombe chotara wana sifa bora mchanganyiko za
ng’ombe wa kigeni na wa asili.

7.1.1. Upandishaji

Ni tendo la ng’ombe dume kumpanda ng’ombe jike aliye kwenye joto. Madume na
majike huwekwa pamoja katika uwiano unaoshauriwa katika kipindi chote cha mwaka na
kwa mtindo huu ndama huzaliwa katika kipindi chote cha mwaka. Upandishaji huu ndio
unaotumika zaidi na wafugaji wa ng’ombe wa asili.
Angalizo:
Hakikisha unapandisha ngo’ombe ili kuwezesha ndama wengine kuzaliwa wakati kuna
malisho na maji ya kutosha.

7.1.2. Kupandisha kwa wakati/muda maalum

Upandishaji kwa wakati maalumu hutumika pale inapotakiwa ng’ombe wengi wapate
mimba na kuzaa kwa wakati mmoja ambapo kuna maji na malisho ya kutosha. Madume
kwa kawaida huchanganywa na majike kwa wakati uliopangwa.

7.1.3. Faida zake.

i. Kurahisisha utunzaji wa ndama kwa kuwa na ndama wengi kuzaliwa kwa wakati
mmoja badala ya ndama mmoja mmoja au wachache kila wakati.
ii. Kulenga soko la mifugo kwa kuzalisha ndama wengi watakao kuwa tayari kuuzwa
kwa wakati mmoja.
iii. Kuoanisha upatikanaji wa malisho mengi na bora zaidi na kuzaliwa kwa ndama
ngo’ombe wakipanda malisho bora na ya kutosha watatoa maziwa kwa wingi,
ndama watakuwa haraka na mazao yanayokusudiwa yanapatikana mapema
iv. Inasaidia kuwatambua ng’ombe kwenye kundi ambao hawapati mimba
Angalizo:
Umakini unahitajika katika kumwondoa ng’ombe ambaye hajapandwa kwa wakati huo.

8.0. UBORESHAJI NA USIMAMIZI WA MALISHO YA ASILI.

Chakula kikuu cha ng’ombeni nyasi na majani jamii ya mikunde ambayo haia madhara kwa
afya ya mnyama.

8.1.0. Malisho ya Asili.

Malisho haya kwa kawaida hukua haraka na kupoteza viinilishe muhimu, kwa muda mfupi
baada ya mvua. Malisho ya asili huwa na viinilishe vinavyotosheleza mahitaji ya mifugo na
wakati wa kiangazi malisho huwa duni na yasiyotosheleza. Wakati malisho yanatosheleza
ng’ombe huwa na uzito wa kuridhisha tofauti na wakati wa kiangazi ambapo ng’ombe
hupungua uzito. Malisho ya asili ya jamii ya nyasi huwa na upungufu wa viinilishe hususani
protini. Mikunde ina tabia yakutopungua viinilishe haraka ikilinganishwa na nyasi.

8.1.1. Malisho yaliyoboreshwa

Malisho ya asili yanaweza kuboreshwa kwa kuongeza mimea aina ya mikunde, kuongeza
nyasi bora kwenye malisho, kuongeza samadi kwenye mbuga za malisho. Malisho
yaliyoboreshwa yana uwezo wa kuwafanya wanyama wakue haraka na kufikia uzito wa
kuchinjwa mapema.

8.1.2. Taratibu za kuboresha malisho/ Mambo ya kuzingatia

i. Uwezo wa kuvumilia hali ya hewa na mazingira yaliyopo
ii. Yawe yenye kuvumilia magonjwa na wadudu waharibifu
iii. Yawe yasiyozidiwa nguvu na magugu
iv. Yawe yenye kustahimili kuchungwa
Inafaa maeneo ya kuchungia/kulishia yatengwe na kugawanywa katika sehemu ambazo
nyasi zitaoteshwa na kukuzwa. Hatimaye nyasi hizo zichungwe kwa nyakati tofauti ili
kuepuka uharibifu na kuhakikisha kuwa nyasi zinatosheleza vipindi vyote vya mwaka.
Utaratibu huo utasaidia pia kupunguza uwezekano wa mifugo kuambukiza magonjwa.

8.1.3. Uhifadhi wa malisho

Malisho hupatikana kwa wingi wakati wa masika, na wakati huo yana ubora unaotakiwa.
Wakati wa masika, mifugo hula malisho na kusaza ambapo wakati wa kiangazi malisho
huwa haba na virutubisho hupungua ili kuwa na uhakika na upatikanaji na chakula cha
kutosha na bora wakati wote, ni muhimu kuhifadhi malisho ya ziada katika kipindi hicho.

8.1.4. Njia za kuhifadhi malisho.

Kuna njia kuu mbili za kuhifadhi malisho nazo ni;
i. Kuyakausha (Hei)
ii. Kuyavundika (Saileji)

8.1.5. Kuyakausha (Hei).

Hei ni majani makavu ambayo yanaweza kulishwa wanyama yangali shambani au kuvunwa
na kufungwa kwenye marobota kisha kuhifadhiwa kwa matumizi ya baadaye. 

8.1.6. Hatua ya kutayarisha

i. Vuna majani yanapoanza kutoa maua
ii. Yaanike na yageuze majani mara moj au mara mbili kwa siku ili yakauke vizuri
iii. Ukaushaji huchukua siku tatu hadi sita kutegemea aina ya majani au hali ya hewa
iv. Majani yakiisha kauka yafunge kwenye marobota
v. Yahifadhi marobota sehemu isiyoingiza mvua au unyevu
vi. Marobota ya majani makavu yanaweza kutengenezwa kwa mashine au kwa
kutumia makasha ya mbao.
vii. Mfugaji mdogo anashauriwa kutumia makasha ya mbao kwa kutengeneza
marobota hayo.
viii. Makasha ya mbao yanaweza kutengenezwa kwa kutumia vipimo vifuatavyo,urefu sentimita 75, upana sentimita 45 na kina sentimita 35.
ix. Majani yaliyofungwa katika marobota hutumia sehemu ndogo ya kuhifadhia na pia
hupunguza upotevu.
x. Mfugaji anaweza kukadiria kiasi cha malisho atakayotumia kulisha ng’ombe wake
kwa msimu wa kiangazi.

8.1.7. Masalia ya mazao shambani

Masalia ya mazao kutoka shambani yanaweza kutumiwa ili kufidia chakula ambacho
ng’ombe amekikosa kutokana na uhaba wa majani wakati wa kiangazi. Masalia yanaweza
kuwa ya mabua ya nafaka mbalimbali kama vile mahindi, mtama, mpunga, ulezi, ngano au
uwele. Mengine ni majani ya viazi vitamu, miwa au majani ya jamii ya mikunde kama vile
maharage,kunde, njugu mawe au mbaazi.
Masalia yanaweza kutumiwa na ng’ombe moja kwa moja bila kuboreshwa. Hata hivyo
ng’ombe hawezi kula kwa wingi na hivyo inashauriwa kuyanyunyuzia molasses au magadi
ili ng’ombe aweze kula mengi zaidi.

8.1.8 .Maji

Maji ni muhimu katika kupoza joto la mwili kutengeneza maziwa, kusafirisha virutubisho
na kutoa uchafu mwilini kwa njia ya mkojo,kinyesi kupumua na jasho. Ng’ombe akipata
maji ya kutosha hukua vizuri, huwa mwenye afya na hutoa maziwa mengi na bora. Kiasi
cha asilimia 85 hadi 87 ya maziwa ni maji. Ng’ombe anapokosa maji hukosa hamu ya kula
na hali hiyo ikiendelea hupungukiwa maji na hupoteza uzito. Ng’ombe anaweza kupata
maji kwa njia zifuatazo;
i. Kunywa
ii. Kula vyakula vyenye maji maji

8.1.9. Vyakula vya ziada

Hakikisha mifugo yako wanapata vyakula vya ziada kama vile
i. Pumba za mahindi, mtama,ngano
ii. Mashudu ya pamba au alizeti
iii. Madini
iv. Vitamini

9.0 SHUGHULI ZA UTUNZAJI BORA WA AFYA YA MIFUGO.

9.1. Uogeshaji.

Mifugo waogeshwe mara kwa mara ili kuepukana na magonjwa yaenezwayo na kupe
pamoja na ndorobo. Uogeshaji unaweza kufanyika kwa kutumia pampu za mgongoni
(knapsack sprayers) au kuwatumbukiza katika josho lililotiwa dawa ya kuogeshea.

9.2. Kuwapa dawa ya minyoo

Mifugo wapatiwe dawa za minyoo mara kwa mara ili kuhakikisha ukuwaji wao na utoaji
wa maziwa uendelee vizuri. Mifugo wapewe dawa za minyoo kila baada ya miezi mitatu

9.3. Kuhasi

Ndama dume wasiohitajika kwa ajili ya kuzalisha baadaye wahasiwe kwa njia ya
operesheni au kwa kutumia koleo au badizo iwapo ndama ni wakubwa.

9.4. Kuwapa ndama alama za utambulisho

Ndama wapewe namba au alama za utambulisho mara wafikiapo miezi 6 tangu kuzaliwa.
Utambulisho unaweza kuwa wa chuma au plastiki chenye nambari kwenye sikio,mikato
maalumu katika masikio au chapa katika sehemu malum za mwili.

9.5. Kuondoa vichomozo vya pembe

Ndama waondolewe pembe katika mwezi wa kwanza tangu kuzaliwa. Tumia chuma cha
moto kuchoma kichomozo chote cha pembe.

10.0. MAZAO YATOKANAYO NA MIFUGO.

Kutokana na ufugaji wa ng’ombe wa asili, tunapata mazao yafuatayo:
i. Nyama
ii. Maziwa
iii. Mbolea
iv. Ngozi
v. Kwato
vi. Mifupa
vii. Damu
viii. Pembe

10.1. Maziwa

Maziwa yanaweza kusindikwa na kupata mazao mengine ya mifugo kama vile samli, siagi
na jibini

10.2. Pembe na kwato

Mazao haya vile vile yanaweza kutumika kutengeneza gundi, vifungo, mapambo na pia
vyombo vya kunywea vinywaji mbalimbali na pia kama tarumbeta.

10.3. Ngozi

Ni zao linaloweza kutumika katika kutengenezea mikanda, viatu na mikoba ya ngozi.

10.4. Damu na Mifupa

Damu na mifupa huweza kutumika kutengenezea vyakula vya kuku na mifugo mingine.
Matumizi mengine ya Ng’ombe wa asili:
i. Wanyama kazi
ii. Kutolea mahali
iii. Kipimo cha utajiri
iv. Ajira
v. Kuongeza kipato
vi. Kinga dhidi ya majanga
vii. Kufanyia matambiko

11.0. UTAMBUZI WA MWANZO WA MAGONJWA YA MIFUGO.

11.1 .Sifa za mnyama mwenye afya

i. Mchangamfu wakati wote macho maang’avu huku mkia na masikio vikimsaidia
kufukuza inzi
ii. Kula na kucheua, kunywa maji vizuri kila siku
iii. Kuonyesha ushirikiano na kutembea pamoja kwenye kundi
iv. Kutembea vizuri
v. Anastuka na kukimbia anapostuliwa na mnyama hatari anapomkaribia kama vile
mbwa mwitu, fisi, chui, simba.
vi. Mwili wake una uwezo mkubwa wa kukibadili chakula anachokula kutoa mazao ya
kutosha kama vile maziwa.
vii. Anaonekana mwenye nguvu na kwa wale wanaoendelea kukuna wanaongezeka
uzito kwa muda mfupi
viii. Kwa mnyama anayekamuliwa mara kwa mara kupiga kelele za kumtafuta mtoto
wake,kiwele huwa kimejaa maziwa, chuchu huwa wakati mwingine zimetanuka
upande kwa ajili ya kujaa maziwa
ix. Ngozi ya mnyama husisimka mara kwa mara wadudu wapomtambaa
x. Kwa madume, huwa wana hamu ya kuwapanda majike wanaoingia kwenye joto.
Miili yao hujengeka vizuri. Pumbu hujengeka na kukaa vizuri kwenye nafasi yake
(yaani katikati ya miguu)
xi. Pua na midomo huwa na unyevu unyevu wakati wote.
xii. Ngozi kuwa na ulaini unaotakiwa na manyoya hung’aa.
xiii. Kwa kawaida unapo mkaribia mnyama endapo amekaa chini ni lazima atanyanyuka

11.2. Dalili za Mnyama anayeumwa

i. Hukosa hamu ya kula na kunywa maji
ii. Mwili kunyong’onyea na kuonekana mchovu
iii. Mnyama kutembea pole pole na kwa taabu na mara nyingi hujitega na wenzake
iv. Pua zake na midomo huonekana kukauka.
v. Kupunguka kwa kiwango cha uzalishaji kama vile maziwa. Kwa madume huduwaa
na kuinamisha shingo chini na kukosa hamu ya kuwapanda majike wanaoingia
kwenye joto.

11.3. Vyanzo vya magonjwa

Magonjwa mengi ya mifugo husambazwa na vijidudu ambao huingia kwenye mfumo wa
damu na kusababisha homa na baadae madhara makubwa. Mangonjwa mengi ya mifugo
husababishwa na vyanzo kutoka nje ya mwili wa mnyama mfano mazingira machafu
anayoishi mnyama, vitu vinavyopelekea vidonda (Vitu vyenye ncha kali) husababisha
vidonda ambapo vimelea vinaweza kukaa.Pia mnyama anaweza kupata ugonjwa kutokana
na hali za ndani ya mwili kama upungufu wa lishe, mfano: madini, na na magonjwa ya
kulithi.
Mfano wa wadudu hao ni;

11.4. Vimelea (bacteria)

Mfano wa magonjwa yanayosababishwa na bacteria ni chambavu, Blackquarter, Kimeta,
Kifua kikuuu, brucellosis (ugonjwa wa kutupa mimba) na ugonjwa wa kiwele.Ng’ombe
dume huvimba mapumbu.

11.5 .Virusi (virus) Otatis

Mfano wa magonjwa yanayosababishwa na virusi ni kichaa cha mbwa (Rabies), Ugonjwa
wa midomo,miguu (foot and mouth disease) na Sotoka (Rinderpest)

11.6. Protozoa

Magonjwa yanayo sababishwa na protozoa ni kama ndigana baridi, ndigana kali, ndigana
mkojo damu, ndigana maji moyo na nagana.
Angalizo:
Magonjwa yote ya Ndigana husambazwa na makupe, wakati ugonjwa wa nagana
husambazwa na ndorobo.

11.7. Lishe duni.

Upungufu wa viinilishe katika chakula cha mifugo husababisha madhara katika mwili kama
ifuatavyo;
i. Husababisha majike kutopata joto mapema
ii. Ndama kuzaliwa na viungo visivyo komaa
iii. Upungufu wa uzalishaji maziwa
iv. Kiwango cha uzalishaji kushuka

11.8. Vidonda/michubuko

Kupitia vidonda au michubuko, wadudu wasababishao magomjwa huweza kuingia mwilini
kwa mnyama

 

11.9. Magonjwa ya kurithi

Kama mmoja wa wazazi ana ugonjwa wa kurithi basi kuna uwezekano mkubwa kwa
mmoja wa ndama watakaozaliwa kurithi ugonjwa huo

12.0. MAGONJWA YANAYOENEZWA NA KUPE.

12.0. Ndigana kali

12.1.1. Dalili zake

i. Homa kali hadi nyuzi joto 42c
ii. Povu kutoka mdomoni na puani
iii. Kuhara choo kilichochanganyikana na kamasi na damu
iv. Tezi kuvimba sana na zenye joto
v. Kuacha kula
vi. Ukungu kwenye macho
vii. Kifo baada ya wiki moja hadi mbili

12.1.2. Tiba.

Butalex, Parvexon, tiba iambatane na sindano moja ya kuondoa uvimbe kwenye mapafu
kama hali hiyo tayari imeshajitokeza. Tumia Multivitamin ili kuongeza hamu ya kula na
Raxis ili kuondoa maji kwenye mapafu.

12.1.3. Kinga/zuia.

Zingatia uogeshaji sahihi na Chanjo ya ECF

12.2.0. Ndigana baridi (Anaplasmosis)

12.2.1. Dalili zake

i. Homa hadi nyuzi joto 42C
ii. Kukosa hamu ya chakula
iii. Choo kigumu na makamasi na harufu mbaya
iv. Kifo baada ya siku 8 hadi 10

12.2.2. Tiba.

i. Antibiotic kama vile Oxytetracycline
ii. Imizol.

12.2.3. Kinga.

Zingatia uogeshaji sahihi

12.3.0 Ndigana mkojo damu (Babesiosis) ugonjwa wa kukojoa damu

12.3.1 Dalili zake

i. Mkojo kuwa na rangi ya damu isiyokolea zambarau
ii. Mkojo hutoka kidogo kidogo na kwa muda mrefu
iii. Homa hadi nyuzi joto 40C
iv. Kuacha kula
v. Choo kigumu au kuhara wakati mwingine
vi. Kifo baada ya wiki 1

12.3.2. Tiba.

Berenil ikisaidiwa na antibiotics za sindano kama vile oxytetracycline (OTC) pia tumia
Multivitamin kuongeza hamu ya kula.

12.3.3. Kinga

Zingatia uogeshaji sahihi

12.4.0. Ndigana maji moyo (heart water)

12.4.1. Dalili zake

i. Kizunguzungu na kuanguka,
ii. Kifo baada ya siku 2

12.4.2.Tiba

Antibiotics za sindano kama vile oxytetracycline. Kumbuka tiba lazima ifanywe mapema
iwezekanavyo

12.4.3. Kinga/kuzuia.

Zingatia uogeshaji sahihi

13.0. UTUNZAJI WA KUMBUKUMBU.

Uwekaji wa kumbukumbu ni muhimu sana kwa kila mfugaji. Kumbukumbu zinasaidia
katika kujua mambo mengi kama matukio ya magonjwa, tiba, chanjona uogeshaji,
gharama za uendeshaji kama gharama za madawa ya tiba, chanjo na uogeshaji, mishahara
ya wafanyakazi, faida au hasara baada ya mauzo. Kumbukumbu hizi humsaidia mfugaji
Kufanya maamuzi katika uendelezaji wa Shamba Lake.

13.1.0. Aina za kumbukumbu

Kumbukumbu muhimu katika ufugaji wa ng’ombe ni pamoja na idadi ya ndama
wanaozaliwa, idadi ya ng’ombe,afya ya ng’ombe,kumbukumbu ya mapato na matumizi.
Hata hivyo mfugaji anaweza kuongeza kumbukumbu nyingine kulingana na mahitaji na
shughuli zake.

B.UFUGAJI BORA WA NG’OMBE WA KISASA.

14.0.NG’OMBE WA NYAMA.

Ng’ombe wanaofaa kufugwa kwa ajili ya uzalishaji nyama ni wale wanaokua kwa haraka na kuweka misuli mikubwa iliyojengeka vizuri.  Baadhi ya koo zenye sifa hizo ni pamoja na Boran, Mpwapwa (nyama na maziwa), Charolais, Aberdeen Angus, pamoja na chotara wao.  Hata hivyo, nchini Tanzania ng’ombe aina ya Zebu (mfano Ufipa,Gofo, Masai, Sukuma, Tarime, Iringa red), Sanga (Ankole) na chotara wao ndio hutumika kama ng’ombe.

14.1.0. Utunzaji  wa ng’ombe wa nyama

Ng’ombe wengi wanaofugwa hapa nchini Tanzania ni wa asili ambao kwa kiwango kikubwa hutumika kwa ajili ya uzalishaji wa nyama.  Hata hivyo uzalishaji wake wa nyama ni mdogo kutokana na kasi ndogo ya kukua na kuwa na uzito mdogo wakati wanapopevuka.  Hali hii husababishwa na matunzo duni, kwa kuwa huchungwa/hulishwa kwa kutegemea malisho peke yake ambayo hayawezi kukidhi mahitaji ya viinilishe vinavyohitajika kwa ng’ombe.

14.1.1. Utunzaji wa ndama

Ili kuongeza kasi ya ukuaji na kuongeza uzalishaji wa nyama, mfugaji anapaswa kufanya mambo yafuatayo:-
v  Wajengewe banda/boma imara safi na lisilo na unyevunyevu ili kuepukana na magonjwa kama kichomi na kuhara
v  Waruhusiwe kunyonya kwa muda usiopungua miezi sita, pia wapatiwe majani laini kuanzia wanapofikia umri wa wiki mbili ili waanze kula mapema.
v  Wapatiwe maji safi na yakutosha
v  Ndama dume ambao hawatahitajika kwa ajili ya kuendeleza kizazi wahasiwe wakiwa na umri wa wiki mbili ili waanze kula mapema.
v  Wapatiwe maji safi na yakutosha
v  Ndama dume ambao hawatahitajika kwa ajili ya kuendeleza kizazi wahasiwe wakiwa na umri usiozidi miezi 3 ili wakue haraka na kuwa na nyama nzuri.
v  Wawekwe alama au namba za utambulisho kati ya siku ya kwanza na ya tano kwa ndama wote, mfano kuvalishwa hereni kwenye masikio, kwa ajili ya urahisi wa udhibiti wa umiliki na utunzaji kumbukumbu.
v  Ndama wachungwe eneo tofauti na ng’ombe wakubwa kuepuka maambukizi ya minyoo na magonjwa na

14.1.2.Utunzaji wa ndama baada ya kuachishwa kunyonya hadi kupevuka (miezi 6 – 24).

Ndama wa umri huu anatakiwa apatiwe:
1)      Malisho bora na maji safi ya kutosha wakati wote
2)      Vyakula vya ziada ili kukidhi mahitaji ya mwili (mifano ya vyakula mchanganyiko imeonyeshwa kwenye jedwali Na. 3 ) na
3)      Tiba na kinga dhidi ya magonjwa hususan kinga ya kutupa mimba (S19) kwa ndama jike watakaotumika kuendeleza kundi.
4)      Katika kipindi cha miezi 6 hadi 24 mfugaji anashauriwa kuchagua ndama watakaoingizwa katika kundi la wazazi na wanaobaki wawe katika kunenepesha kwa ajili ya nyama.

14.1.3.Unenepeshaji wa ng’ombe wakubwa.

Ng’ombe kwa ajili ya nyama anaweza kuchinjwa akiwa na umri wa kuanzia miezi 3 kulingana na mahitaji ya soko.  Kwa kawaida hapa Tanzania ng’ombe huchinjwa wakiwa na umri wa kuanzia miezi 18 kwa ng’ombe wa kigeni na zaidi ya miezi 36 kwa ng’ombe wa kigeni na zaidi ya miezi 36 kwa ng’ombe wa asili.

14.1.4.Mkulima atapata faida kwa kuzingatia yafuatayo.

Ili mfugaji aweze kupata faida kutokana na ufugaji wa ng’ombe wa nyama anapaswa afanye yafuatayo:-
1)      Afuge aina ya ng’ombe wanaokua na kukomaa haraka
2)      Anenepeshe ng’ombe kwa muda wa miezi 3 – 6 kabla ya kuchinjwa.  Unenepeshaji huongeza ubora wa nyama na kipato kwa mfugaji.
3)      Awapatie chakula chenye mchanganyiko wenye viinilishe vya kutosha viinilishe vya kutia nguvu na joto mwilini viwe na uwiano mkubwa kuliko vingine (Jedwali Na.3), na
4)      Auze ng’ombe mara wanapofikisha umri na uzito unaohitajika katika soko ili kuepuka gharama za ziada.

     Jedwali na.1. Mfano wa mchanganyiko wa chakula kwa ajili ya unenepeshaji.


AINA YA CHAKULA
KIASI KWA KILO
Majani makavu ya mpunga/NganoHey
23.3
Molasis
44.72
Mahindi yaliyorazwa
18.94
Mashudu ya Alizeti/pamba
11.4
Madini mchanganyiko
0.7
Chumvi
0.47
Urea
0.47
Jumla
100

14.2.0. Malisho bora na vyakula vya ziada.

14.2.1.Uzalishaji na uhifadhi wa malisho bora na vyakula vya ziada.

Chakula kikuu cha ng’ombe ni nyasi, vyakula vingine ni pamoja na miti malisho, mikunde na mabaki ya mazao.  Ili kupata malisho misimu yote ya mwaka ni muhimu kuvuna na kuhifadhi malisho kipindi yanapopatikana kwa wingi.  Inawezekana kupanda malisho mengi kuliko kiasi kinachohitajika msimu mmoja/wakati wa mvua, kuyavuna yanapofikia hatua ya kutoa maua na kuyahifadhi (mfano wa malisho yanayoweza kupandwa ni mabingobingo, Guatemala, African fox-tail, desmodium, centrosema, lukina n.k).  Malisho yakupandwa ni vizuri yawe na mchanganyiko wa jamii ya nyasi, mikunde na miti malisho.



14.2.2.Masalia ya mazao shambani.

Masalia ya mazao shambani kama vile mabua, magunzi, majani ya mikunde, viazi, ndizi, mpunga, na mengineyo yanaweza kukusanywa na kuhifadhiwa vizuri kama chakula cha ng’ombe.

14.2.3.Malisho ya miti na matunda yake.

Malisho yatokanayo na miti ya malisho na matunda yake yanaweza kutumika kama malisho ya ng’ombe.  Majani na matunda ya miti ya lukina, sesibania, migunga na mbaazi yanaweza kukaushwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kulisha ng’ombe.

14.2.4.Vyakula vya ziada

Ili kukidhi mahitaji ya viinilishwe kulingana na kiwango cha uzalishaji, ng’ombe anatakiwa kupewa vyakula vya ziada.  Vyakula hivyo vinatokana na mchanganyiko wa vyakula mbalimbali.  Michanganyiko hii  inategemeana na upatikanaji wa malighafi katika maeneo husika.  
Mifano ya mchanganyiko huo ni kama ifuatavyo:-

Jedwali na.2 Mfano wa kwanza wa chakula cha ziada

AINA YA CHAKULA
KIASI (KILO)
Pumba za mahindi
47
Mahindi yaliyoparazwa
20
Mashudu ya alizeti/pamba
20
Unga wa lukina
10
Chokaa ya mifugo
2
Chumvi
1
Jumla
100


Mfano wa pili wa chakula cha ziada ni tofali la kulamba lenye urea ambalo mchanganyiko wake ni:-

Jedwali na. 3. Mfano wa kwanza wa chakula cha ziada

NGOMBE
WALIOACHA KUNYONYA.(KG)
WA MAZIWA (KG)
1
Pumba za mahindi
66
56
2
Pumba laini za mpunga
-
10
3
Mashudu ya alizeti(meusi)
25
25
4
Chokaa
3
3
5
Mifupa iliyochomwa na kusagwa
3.5
3.5
6
Chumvi
1
1
7
Madini yenye colt+salfa
1.5
1.5

JUMLA
100
100

 

 

14.2.4.Mambo mhimu ya kuzingatia.

Mfugaji anatakiwa kuzingatia yafuatayo ili kupata tija katika ufugaji:-
v  kulisha mchanganyiko wa nyasi, mikunde na mchanganyiko wa madini na vitamin
v  kutenga maeneo kwa ajili ya kulisha ng’ombe kwa mzunguko pamoja na kupanda malisho katika mfumo huria na nusu huria na
v  kuvuna nyasi na mikunde inapofikia hatua ya kutoa maua na kuyahifadhi kwa matumizi wakati wa uhaba wa malisho hususan wakati wa kiangazi.

14.2.4.0.Njia za kuhifadhi malisho

Malisho yanaweza kuhifadhiwa kwa kuyakausha (Hei) au kuyavundika (Sileji).

14.2.4.1.Hei

Hei ni majani yaliyohifadhiwa kwa kukaushwa baada ya kukatwa au kuachwa kukauka yakiwa shambani kwa matumizi ya baadaye.  
Katika kutengeneza hei yafuatayo yazingatiwe:-
1)      Vuana malisho yanapoanza  kutoa maua
2)      Yaanikwe kwa siku 3 hadi 6 kutegemea aina ya malisho na hali ya hewa na yageuze mara 1 au 2 kwa siku ili yakauke vizuri.
3)      Yafungwe katika marobota baada ya kukauka inawezekana kutumia kasha la mbao lenye vipimo vifuatavyo:-  Urefu sentimeta 75, upana sentimeta 45 na kina sentimeta 35 au mashine na zana za kufunga marobota ya hei na
4)      Hifadhi marobota juu ya kichanja ili kuzuia maji yasiingie unyevu na kuharibiwa na wadudu.

 

 

14.2.4.2.Sileji.

Sileji ni majani yaliyokatwakatwa na kuvundikwa.  Madhumuni ya kuyavundika ni kuyawezesha kubaki na ubora wake hadi wakati yatakapotumika katika kutengeneza sileji yafuatayo yazingatiwe:-
v  Tengeneza sileji kwa kutumia majani yenye sukari nyingi kama mahindi au mabingobingo na mikunde, mabaki ya viwandani kama molasis,
v  Andaa shimo au mfuko wa plastiki kulingana na kiasi cha majani yaliyovunwa.
v  Vuna majani ya kuvundika katika umri wa kuanza kutoa maua.  Endapo majani yaliyovunwa ni teketeke yaachwe kwa siku moja yanyauke kupunguza kiwango cha maji.
v  Katakata majani uliyovuna katika vipande vidogovidogo,
v  Tandaza majani uliyokatakata ndani ya shimo au mfuko katika tabaka nyembamba na kushindilia ili kuondoa hewa yote.
v  Funika shimo ulilojaza majani kwa plastiki ikifuatiwa na udongo.
v  Sileji itakuwa tayari kutumika kuanzia siku 21 na
v  Sileji iliyofunguliwa kwa ajili ya matumizi ifunikwe haraka iwezekanavyo ili kuzuia kuharibika.
v  Sileji inaweza kubaki na ubora katika shimo kwa muda mrefu kama haitafunguliwa na kuachwa wazi kwa muda mrefu.

15.0. NG’OMBE WA MAZIWA.

15.1.0.Sifa za ng’ombe wa maziwa zifuatazo:-

Ø  Umbo lililopanuka kwa nyuma na kupungua kuelekea kichwani.
Ø  Mgongo ulionyooka kuanzia mabegani kuelekea mkiani
Ø  Miguu ya nyuma mirefu iliyonyooka, minene yenye kuacha nafasi kwa ajili ya kiwele na kwato imara.
Ø  Kiwele kiwe kikubwa chenye chuchu nne, ndefu na unene wa wastani
Ø  Nafasi kati ya chuchu na chuchu iwe ya kutosha na
Ø  Endapo ng’ombe anakamuliwa awe na kiwele kikubwa kilichoshikamana vizuri mwilini, na mishipa mikubwa kwenye kiwele iliyosambaa.
Aina ya ng’ombe wa maziwa wanaofugwa kwa wingi nchini ni pamoja na Friesian, Ayrshire, jersey, Mpwapwa, Simmental na chotara watokanao na mchangoayiko wa aina hizo na Zebu.

16.0.UTUNZAJI WA MAKUNDI MABALIMBALI YA NG’OMBE WA MAZIWA KULINGANA NA UMRI NA HATUA YA UZALISHAJI



16.1.0.Utunzaji wa ndama

Mfugaji anapaswa kutunza ndama vizuri kwa lengo la kupata ng’ombe wengi na bora kwa ajili ya maziwa.  Mambo muhimu ya kuzingatia katika utunzaji wa ndama tangu kuzaliwa hadi kuachishwa maziwa ni pamoja na
Ø  Kuhakikisha kuwa ndama anapakwa dawa ya kuzuia maambukizi ya viini ya magonjwa kupitia kwenye kitovu, kwa mfano dawa joto (Tincute of Iodine) mara baada ya kuzaliwa na
Ø  Ndama apatiwe maziwa ya awali yaani dang’a (colostrums) mara baada ya kuzaliwa kwa lengo la kupata kinga ya mwili dhidi ya magonjwa.  Aidha, aendelee kunyonya maziwa hayo kwa muda wa siku 3-4.

16.1.1.Utenganezaji wa maziwa kwa ajili ya ndama.

Endapo jike aliyezaa amekufa au hatoi maziwa, apewe dang’a toka kwa ng’ombe mwingine kama yupo au dang’a mbadala, ambayo inaweza kutengenezwa kwa kuchanganya vitu vifuatavyo:-
Lita moja ya maziwa yaliyokamuliwa wakati huohuo.
Lita moja ya maji yaliyochemshwa na kupozwa hadi kufikia joto la mwili.
Kijiko kimoja cha chai cha mafuta ya samaki (cod liver oili).
Mafuta ya nyonyo vijiko vya chai 3 na
Yai moja bichi.
Koroga mchanganyiko huo, weka katika chupa safi.

16.1.2.Unyweshaji wa maziwa kwa ndama.

Ndama anyweshwe kabla haujaopoa.  Ndama anyweshwe mchanganyiko huo mara 2 kwa siku kwa muda wa siku 3 mfululizo na kila mara mchanganyiko uwe mpya.  Wakati wa kunywesha chupa iwekwe juu ya  kidogo ili asipaliwe.Endapo ndama hawezi kunyonya ng’o mbe akamuliwe na ndama anyweshwe maziwa kwa njia ya chupa kwa kuzingatia usafi wa maziwa na chupa.Ndama aendelee kunyweshwa maziwa kwa kiasi kama ilivyoonyeshwa kwenye Jedwali Na. 1. Ndama aanze kuzoeshwa kula nyasi laini, pumba kidogo na maji safi wakti wote kuanzia wiki ya 2 baada ya kuzaliwa na ndama aachishwe kunyonya au kupewa maziwa akiwa na umri wa miezi 3.  Mfugaji ahakikishe kwamba ndama anayeachishwa kunyonya ana afya nzuri.

Jedwali na. 4. Kiasi cha maziwa na chakula maalumu kwa ndama.

UMRI (WIKI)
KIASI CHA MAZIWA KWA SIKU (LITA)
KIASI CHA CHAKULA MAALUM CHA NDAMA KWA SIKU (KILO)
1
3.0
0.0
2
3.5
0.0
3
4.0
0.0
4
4.5
0.0
5
5.0
0.1
6
5.0
0.2
7
5.0
0.3
8
4.0
0.4
9
3.0
0.7
10
2.0
1.0
11
1.5
1.25
12 - 16
0.75
1.5

Vyombo vinavyotumika kulishia ndama visafishwe vizuri kwa maji yaliyochemshwa, sabuni na kukaushwa.

16.1.2.Matunzo mengine ya ndani ni pamoja na:-

a)      Kuondoa pembe kati ya siku 3 hadi 14 mara zinapojitokeza ili kuzuia wanyama kuumizana na kuharibu ngozi,
b)      Kukata chuchu za ziada kwa ndama jike
c)      Kuhasi ndama dume wasiozidi umri wa miezi 3 ambao hawatahitajika kwa ajili kuendeleza kizazi ili wakue hawatajika kwa ajili ya kuendelea kizazi ili wakue haraka na kuwa na nyama nzuri.
d)     Kuweka alama au namba za utambulisho kati ya siku ya kwanza na ya tano, mfano kuvalishwa hereni kwenye masikio kwa ajili ya urahisi wa udhiti wa umiliki na utunzaji kumkukumbu na,
e)      Kuwapatia kinga dhidi ya maabukizi na tiba ya magonjwa wanapougua.
Kumbuka:Huduma hizi zifanyike chini ya maelekezo ya mtaalam wa mifugo.

16.2.0.Utunzaji wa ndama baada ya kuachishwa maziwa hadi kupevuka (miezi – 18)

v  Ndama baada ya kuachishwa maziwa apate malisho bora na chakula mchanganyiko kuanzia kilo 2 4 kwa siku kutegemea umri wake na
v  Ndama wanapofikia umri wa miezi 18 wachaguliwe wanaofaa kuendeleza kizazi, wasio na sifa nzuri waondolewe katika kundi.

16.2.1.Utunzaji wa mtamba

Mtamba ni ng’ombe jike aliyefisha umri wa kupandwa (wastani wa miezi 18) hadi anapozaa kwa mara ya kwanza.  Ni muhimu kutunza vizuri mtamba ili kupata kundi bora la ng’ombe.  Miezi 3 kabla ya kupandishwa mtamba apatiwe:-
v  Malisho bora
v  Maji ya kutosha
v  Madini  mchanganyiko na
v  Chakula cha ziada kiasi cha kilo 2 – 3 kwa siku, ili kuchochea upevukaji na kuongeza uzito wa mwili.

16.3.0.Utunzaji wa ng’ombe wakubwa

Kundi hili linajumuisha ng’ombe wenye mimba, wanaokamuliwa na madume.  Mfugaji anapaswa kutunza vizuri ng’ombe wake wakubwa kwa lengo la kumpatia malisho bora na maji safi ya kutosha kila siku.  Mambo muhimu ya kuzingatia katika utunzaji wa ng’ombe wakubwa ni pamoja na:-
-           Ng’ombe apatiwe majani makavu (hei) wastani wa kilo 10 au majani mabichi kilo 40 kwa siku kutegemeana na uzito.  Iwapo malisho hayatoshi hususan wakati wa kiangazi apewe masalia ya mazao (viwandani na mashambani) kama molasisi, mabua, maharage, mpunga n.k
-          Ng’ombe apewe vyakula vya ziada (pumba, mashudu, madini mchanganyiko, unga wa mifupa na chokaa) kulingana na hatua na kiwango cha uzalishaji na
-          Ng’ombe apatiwe kinga na tiba ya magonjwa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.


17.0.UPANDISHAJI.

Mfugaji anapaswa kumpandisha ng’ombe kwa umri na wakati muafaka ili kuepuka matatizo ya uzazi na pia kuhakikisha anapata ndama bora na maziwa mengi. 

17.1.0. Mambo muhimu ya kuzingatia katika upandishaji.

Mambo muhimu ya kuzingatia ni pamoja na:
v  Mtamba apandishwe akiwa na umri wa miezi 17 -24 na uzito wa kilo 230 – 300 kwa ng’ombe wa kigeni na umri wa miezi 30 – 36 na uzito wa kilo 200 kwa ng’ombe wa asili.  (Rejea jedwali Na 2)
v  Ng’ombe aliyekwisha zaa apandishwe siku 60 baada ya kuzaa na
v  Siku 18 – 23 baada ya kupandishwa, ng’ombe achunguzwe kama ana dalili za joto ili apandishwe tena.  Iwapo ng’ombe ataendelea kuonyesha dalili za joto baada ya kupandishwa mara tatu mfugaji apate ushauri wa mtaalam wa mifugo.

Jedwali na.5.  Umri na uzito unaoshauriwa kupandisha mtamba

AINA YA NG’OMBE
UZITO (KG)
UMRI (MIEZI)
Friesian
240 – 300
18 – 24
Ayrshire
230 – 300
17 – 24
Jersey
200- 250
18 – 20
Mpwapwa
200 – 250
18 – 20
Chotara
230 – 250
18 – 24
Boran
200 – 250
24 - 36
Zebu
200
30 -36

Ni muhimu mfugaji akazitambua dalili za ng’ombe anayehitaji kupandwa ili aweze kumpandisha kwa wakati.  Dalili hizo ni pamoja na
Ø  Kupiga kelele mara kwa mara
Ø  Kutotulia/kuhangaika
Ø  Kutokwa na ute mweupe usiokatika ukeni
Ø  Kupenda kupanda wenzake na husimama akipandwa na wenzake na
Ø  Kunusanusa ng’ombe wengine
Ø  Ng’ombe akionyesha dalili za joto apandishwe baada ya masaa 12, kwa kuhimilisha au kwa kutumia dume bora (kwa mfano, akionyesha dalili asubuhi apandishwe jioni na akionyesha dalili jioni apandishwe asubuhi).

17.3.0.Uhimilishaji.

Uhimilishaji ni njia ya kupandikiza mbegu kwa ng’ombe jike kwa kutumia mrija.  Faida za uhimilishaji ni pamoja na kusambaza mbegu bora kwa haraka na kwa gharama nafuu, kupunguza gharama za kutunza dume na kudhibiti magonjwa ya uzazi.

17.3.1. Mambo ya kuzingatia ili mkulima afaidike.

Ili mfugaji anufaike na huduma hii anapaswa kufanya yafuatayo:-
Ø  Kuchunguza kwa makini ng’ombe mwenye dalili za joto
Ø  Kumjulisha mtaalam wa uhimilishaji mapema ili kuwezesha zoezi hili kufanyika kwa wakati.
Ø  Kuchunguza kama ng’ombe atarudi kwenye joto siku ya 18 – 23 baada ya kupandishwa na
Ø  Ng’ombe aliyepandishwa apimwe mimba siku 60 hadi 90 baada ya kupandishwa.

17.4.0.Matunzo ya ng’ombe mwenye mimba

Ng’ombe mwenye mimba huchukua miezi 9 hadi kuzaa.  Katika kipindi hicho chote anastahili kupatiwa lishe bora na maji ya kutosha ili akidhi mahitaji ya ndani aliye tumboni na kutoa maziwa mengi baada ya kuzaa.

17.4.1.Matunzo ya ng’ombe mwenye mimba.

Mambo ya kuzingatia ni pamoja na
Ø  Ng’ombe apewe lishe bora na maji ya kutosha kipindi chote cha mimba
Ø  Miezi 2 kabla ya kuzaa apewe kilo 2 za chakula cha ziada kwa siku
Ø  Apewe kinga dhidi ya maambukizi na tiba ya magonjwa
Ø  Ng’ombe anayekaribia kuzaa, hususani mtamba, azoeshwe kuingia kwenye sehemu ya kukamulia.

17.5.0.Dalili za ng’ombe anayekaribia kuzaa

Mfugaji anapaswa kufahamu dalili za ng’ombe anayekaribia kuzaa ili aweze kufanya maandalizi muhimu. 

 17.5.1.Dalili zake.

Dalili hizo ni pamoja na
1)      Kujitenda kutoka kwa wenzake
2)      Kiwele kuongezeka 
3)      Chuchu kutoa maziwa zikikamuliwa
4)      Kutokwa na ute mwekundu na sehemu za uke kuvimba na kulegea
5)      Kuhangaika kulala chini na kusimama na
*       Kati ya saa moja hadi mbili kabla ya kuzaa sehemu ya uke hutokwa na maji mengi ambayo husaidia kulainisha njia ya ndama kupita.

 

17.6.0.Huduma kwa ng’ombe anayezaa.

Ng’ombe anayezaa anahitaji uangalizi wa karibu ili kuhakikisha usalama wa ng’ombe na ndama anaezaliwa. 

17.6.1.Mambo ya kuzingatia kwa huduma za ng’ombe anaezaa.

 Mambo ya kuzingatia ni pamoja na yafuatayo:-
a)      Sehemu ya kuzalia ng’ombe iandaliwe kwa kuwekwa nyasi kavu na laini na iwe safi.
b)      Ng’ombe ahamishwe sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuzaa mara baada ya dalili za kuzaa kuonekana
c)      Ng’ombe aachwe azae mwenyewe bifa usumbufu

17.6.2.Maswala ambayo mkulima anahitaji msaada wa kitaalamu.

Mfugaji apate ushauri/huduma kutoka kwa mtaalam iwapo matatizo yafuatayo yatajitokeza:-
v  Ng’ombe kushindwa kuzaa kwa masaa mawili hadi matatu baada ya chupa kupasuka
v  Kondo la nyuma kushindwa kutoka masaa sita baada ya kuzaa
v  Kizazi kutoka nje na
v  Ng’ombe kushindwa kusimama baada ya kuzaa

17.6.0.Matunzo ya ng’ombe anayekamuliwa.

Ng’ombe anayekamuliwa anahitaji kupata chakula kwa ajili ya kujikimu na cha ziada kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa.  Ili kukidhi mahitaji ya uzalishaji wa maziwa ng’ombe:
a)      Apewe chakula cha ziada kwa kiwango cha kilo 1 kwa kila lita 2 – 3 za maziwa anayotoa.
b)      Apewe madini na virutubisho vingine kulingan ana mahitaji
c)      Apewe maji mengi kwa vile ni ya muhimu katika kutengeneza maziwa.
d)     Aachwe kukamuliwa siku 60 kabla ya kuzaa.  Uachishwaji huu ufanywe taratibu ili ifikapo siku ya 60 kabla ya kuzaa ukamuaji usitishwe.
e)      Baada ya kusitisha kukamuliwa apewe kilo 2 za chakula cha ziada kwa siku hadi atakapozaa na
f)       Apatiwe kinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa na tiba kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.

17.7.0.Uzalishaji wa maziwa.

Lengo la ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ni kupata maziwa mengi, safi na salama pamoja na mazao yatokanayo na maziwa .
Mambo muhimu ya kuzingatia ni:-
Ø  Sehemu ya kukamulia iwe safi na yenye utulivu
Ø  Ng’ombe awe na afya nzuri msafi na kiwele kioshwe kwa maji safi ya uvuguvugu.
Ø  Mkamuaji  awe msafi kucha fupi na asiwe na magonjwa ya kuambukiza
Ø  Inashauriwa mkamuaji asibadilishwebadilishwe
Ø  Vyombo vya kukamulia viwe safi
Ø  Muda wa kukamua usibadilishwe.
Ø  Maziwa ya mwanzo kutoka kila chuchu yakamuliwe kwenye chombo maalum (strip cup) ili kuchunguza ugonjwa wa kiwele.

17.8.0. Uchaguzi wa utunzaji wa dume bora la mbegu.

Dume ndilo linalojenga ubora wa kundi  la ng’ombe katika masuala ya uzalishaji kutokana na uwezo wake wa kupanda majike 20 – 25 wakati wa msimu wa uzalianaji (breeding season).
Ili kundi la ng’ombe liwe bora, mambo yafuatayo yazingatiwe
1)      Chagua dume kutoka kwenye ukoo ulio bora kwa kuzingatia kumbukubu za uzalishaji wa maziwa au nyama za wazazi wake.
2)      Mfugaji apate ushauri wa mtaalam wa mifugo katika kuchagua dume bora
3)      Lisha dume malisho bora na maji safi ya kutosha.  Pia apatiwe chakula cha ziada.
4)      Katika ufugaji shadidi dume la ng’ombe  lifugwe kwenye banda imara lenye sehemu za kuwekea chakula maji na kufanyia mazoezi.
5)      Katika ufugaji huria dume atengewe sehemu na kupatiwa chakula cha ziada.
6)      Dume livalishwe pete puani kwa ajili ya kupunguza ukali na kuwezesha urahisi wa kumshika.
7)      Dume apatiwe kinga na tiba ya magonjwa kulingan ana ushauri wa mtaalam wa mifugo na
8)      Mfugaji apate ushauri wa mtaalam wa mifugo katika kuchagua dume bora.

18.0. UDHIBITI WA MAGONJWA YA NG’OMBE.

Magonjwa huweza kusababishwa na matunzo hafifu lishe duni na visababishi vya magonjwa kama vile protozoa bacteria.
Virusi, riketsia na minyoo.  Aidha wadudu kama kupe na mbung’o wanasambaza visababishi vya magonjwa.

18.1.0. Afya bora ya ng’ombe.

Afya bora ya ng’ombe inatokana na kuzingatia mambo yafuatayo:-
v  Ndama apate maziwa ya awali (dang’a) ya kutosha kwa siku 3 – 4 baada ya kuzaliwa ili kuongeza kinga ya magonjwa mwilini.
v  Chovya kitovu cha ndama ndani ya madini joto (Tincture of Iodine) mara baada ya kuzaliwa kuzuia kuvimba kitovu kutokauka au kutohudumiwa ipasavyo mara baada ya ndama kuzaliwa.  Kitovu huvimba na kutoa usaha hukojoakwa shida na wakati mwingine huvimba viungo.
v  Ndama apewe dawa ya kuzuia minyoo kila baada ya miezi 3 kama atakavyoshauri mtaalam wa mifugo.  Minyoo huwashambulia ndama zaidi hasa wale walioana kula majani.
v  Zingatia usafi wa vyombo na band a epuka kumpa ndama maziwa yaliyopoa na machafu ili kuzuia kuharisha.
v  Zingatia ujenzi wa mabanda kuruhusu mzunguko wa hewa ili kuzuia ndama kupata ugonjwa wa vichomi.  Vichomi huwapata ndama wa umri wa miezi 5 au zaidi wanaofugwa ndani katika mabanda machafu yasiyo na mzunguko wa hewa ya kutosha.
v  Ogesha ng’ombe kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo ili kuua kupe wote wanaoleta magonjwa yatokana yo na kupe (ndigana kali na baridi, kukojoa damu na maji moyo) na mbung’o (ndorobo) na
v  Ng’ombe wapatiwe chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali chanjo muhimu ni za ugonjwa wa kutupa mimba, kimeta, ugonjwa wa miguu na midomo na chambavu.

18.2.0.Msaada wa kitaalamu.

Mfugaji anashauriwa kutoa taarifa kwa mtaalam wa mifugo anapoona ng’ombe wake ana baadhi ya dalili zifuatazo:-
Ø  Joto kali la mwili na manyonya kusimama
Ø  Amepunguza hamu ya kula
Ø  Amezubaa na kutoa machozi
Ø  Anasimama kwa shind ana kusinzia
Ø  Anapumua kwa shida na pua kukauka
Ø  Anatokwa na kamasi nyingi
Ø  Anajitenga na kundi
Ø  Anaconda na
Ø  Anapunguza utoaji wa maziwa ghafla

18.3.0.Dalili za magonjwa na toba.

Kwa dalili za magojwa na tiba zake,tafadhli rejea kipengele cha magonjwa yanayoenezwa na kupe kwa ng’ombe wa asili,kwani magojwa hayo huingiliana.

19.0.KUMBUKUMBU NA TAKWIMU MUHIMU

Kumbukumbu ni taarifa au maelezo sahihi yaliyoandikwa kuhusu matukio muhimu ya kila ng’ombe na shughuli zote zinazohusiana na ufugaji.  Mfugaji anashauriwa kuweka kumbukumbu na takwimu muhimu katika shughuli zake za ufugaji wa ng’ombe.  Kumbukumbu zinamsaidia mfugaji kujua mapato na matumizi na kufanya maamuzi sahihi kuhusu mifugo husika na mifugo husika na mazao yake.  Aidha humwezesha kuweka mipango ya shughuli zake. 
 Mfugaji anapaswa kuweka kumbukumbu muhimu zifuatazo:-
Uzazi (uhimilishaji na matumizi ya dume, tarehe ya kupandwa, kuzaa kuachisha kunyonya)
v  Kinga na tiba
v  Utoaji wa maziwa

v  Ukuaji

4 comments:

  1. ndama wa kike anatakiwa afike umri gani ndo apandwe ...na nikitaka dume 1 ambaye ni mbegu nzuri na jike moja mbegu nzuri inaweza kuwa kiasi gani

    ReplyDelete
  2. Asante sana kwa elimu hii

    ReplyDelete
  3. Ili nipate ndama jike nifanyeje?

    ReplyDelete